Akili Mali

Wito Serikali iwezeshe wakulima wadogo kutumia sola kwa uzalishaji

February 20th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imetakiwa kuwawezesha wakulima wadogowadogo kutumia kawi endelevu yenye gharama nafuu ili kuwapunguzia gharama ya uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Hii ni kufuatia kupanda kwa bei ya kawi ya kawaida kama vile umeme kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na viwango vya ushuru vya juu vya ushuru vinavyotozwa bidhaa hiyo.

“Kwa hivyo, kwa kuwa hitaji la umeme miongoni mwa wakulima linaongezeka kila uchao, matumizi ya kawi safi endelevu ni muhimu katika kutimiza lengo hili kupitia mpango wa kuendeleza matumizi ya kawi endelevu (PURE),” akasema Naibu Mkurugenzi wa Shirika la World Resource Institute (WRI)-Afrika Rebekah Shirley.

Kwa upande wake, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alisema kuwa matumizi ya kawi safi yanaweza kuwasaidia kuimarisha uzalishaji.

“Katika kaunti yangu ya Makueni ambako asilimia 80 ya wakulima ni wale wa mashamba madogomadogo, matumizi ya nishati hii yatawasaidia kutengeneza faida ya Sh1,000 kwa kila siku. Kwa hivyo, serikali inafaa kuwasaidia kwa kuwezesha kumudu bei ya mitambo ya kunasa kawi safi kama vile ya Sola,” akasema.

Gavana Mutula Junior ni miongoni mwa wadau waliohudhuria mkutano wa wadau katika Mpango wa Kuendeleza Matumizi wa Kawi Endelevu (PURE) katika sekta ya kilimo.

Mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Radisson Blue, Nairobi, Februari 7, 2024, ulidhaminiwa na shirika la World Resource Institute (WRI), Kituo cha Utafiti kuhusu Kawi katika Chuo Kikuu cha Strathmore, Wakfu wa Good Energies miongoni mwa wadau wengine katika nyanja ya matumizi ya kawi safi kuendeleza kilimo.

Gavana Mutula Junior alipendekeza kuwa serikali ya kitaifa ipunguze viwango vya ushuru kwa mitambo ya kunasa kawi ya jua ili kuwawezesha wakulima wadogowadogo kuimudu.

“Hii itawezekana kupitia Sheria ya Fedha ya 2024 itakayoandaliwa na kujadiliwa bungeni baadaye mwaka huu 2024,” akasema.

Washiriki walitambua kwamba sekta za kilimo, misitu na uvuvi huchangia asilimia 17.3 ya utajiri katika mataifa yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara kuashiria umuhimu wa sekta hizo katika ustawi wa kiuchumi na maendeleo katika nchi hizo.

“Kwa hivyo, kuendelezwa kwa matumizi ya kawi katika sekta hizi kunaweza kuchangia ukuaji wa kiuchumi, kuimarishwa kwa uzalishaji wa chakula toshelezi na uboreshaji wa maisha ya wakazi wa mashambani kupitia uwepo wa nafasi za ajira na uimarishwaji wa mapato yake,” akasema Bi Wanjira Maathai, Mshirikishi wa WIRA-Afrika.