Habari MsetoSiasa

Wito Shaban awanie wadhifa wa Naibu Rais hapo 2022

September 8th, 2018 1 min read

NA KNA

KUNDI moja la wanasiasa wanawake kutoka Pwani linampigia debe mbunge wa Taveta, Dkt Naomi Shaban kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi wa 2022.

Wakiongozwa na Waziri Msaidizi katika Wizara ya Huduma kwa Umma, Vijana na Jinsia, Bi Rachael Shebesh, viongozi hao walisema wakati sasa umefika kwa nchi hii kuwa na naibu rais mwanamke.

Walimsifia mbunge huyo kama ‘anayefaa zaidi’ kwa kazi ya unaibu rais au uwazir, kutokana na uzoefu wake kisiasa, juhudi za kupigania haki za binadamu na kuwapa motisha wanawake.

Viongozi wengine waliommiminia sifa ni pamoja na mbunge wa Likoni Mishi Mboko, mbunge wa Ijara Sofia Abdi na aliyekuwa Naibu Gavana wa Mombasa Hazel Katana.

Wanasiasa hao walisema hayo mjini Taveta mnamo Ijumaa walipokuwa wakiendesha kampeni ya Huduma Mashinani ambapo wakazi 600 walipokea vyeti vyao vya kuzaliwa, kadi za NHIF, vyeti vya usajili wa biashara na fomu za kuomba mikopo ya benki.

Wakihutubia wakazi, Bi Shebesh ambaye alisema alikuwa anahutubu kwa fursa yake kama mwanamke, alisema Dkt Shaban amedhihirishia wananchi kuwa mwanasiasa mkakamavu mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 20 akipigania haki za wanawake na watoto.

”Tunachosema ni kuwa Naomi Shebesh atatwaa nafasi ya afisi kubwa kama ya naibu rais au waziri mkuu wa Kenya,” akasema waziri huyo.

Viongozi hao waliteta kuwa wanawake wenye maono katika afisi kuu serikalini wamekuwa wakihujumiwa na watu ambao bado wanaamini mwanamke anafaa kuwa chini ya mwanamume.

Akirejelea masaibu yanayomkumba Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bi Beatrice Elachi, Bi Shebesh alisema wanawake wachapakazi wamekuwa wakionekana kama tishio kwa wanaume, na kuzua kampeni potovu za kuwang’oa mamlakani.