Wito viongozi wa kisiasa wasitishe kampeni za mapema

Wito viongozi wa kisiasa wasitishe kampeni za mapema

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuhakikisha kuna amani Kenya inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.

Wachungaji wapatao 100 kutoka Kaunti ya Kiambu, walikongamana katika kanisa la Thika Calvary Church lililoko mjini Thika ili kuiombea nchi.

Askofu mkuu wa kanisa hilo Dkt David Kariuki Ngari ‘Gakuyo’ aliongoza wachungaji wengine kwa kuiombea nchi ili iendeshe uchaguzi wa amani ifikapo mwaka wa 2021.

Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kumrudia Mungu ili aamulie Kenya mustakabali mwema na Wakenya wawe na umoja pamoja na upendo.

“Tunaelewa vyema ya kwamba baadhi ya viongozi wengi wameanza kuendesha kampeni zao za mapema, na kwa hivyo ni muhimu kumrudia Mwenyezi Mungu ili atuongoze kama viongozi nasi tuwaekekeze waumini wetu katika mwelekeo ufaao, ” alifafanua mchungaji huyo.

Dkt Ngari alitoa ujumbe wake kwenye kitabu cha Yeremia 17:14 unaosema: “Niponye Ewe Mungu wangu na nitaweza kupona, na pia niokoe na nitaweza kuokoka kutokana na Imani yangu rohoni”.

Alitoa wito kwa wakenya wote popote walipo wadumishe amani nchini ili tuweze kuwa na uchaguzi wa amani na uwazi.

Aliyasema hayo mjini Thika mnamo Jumatatu wakati wachungaji hao walikongamana huko kanisani ili kuiombea nchi.

“Wakenya wote popote pale walipo wanatarajia kwamba uchaguzi utakuwa wa amani usio na fujo na vurugu,” alisema Dkt Ngari na kuongeza “kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya ili kuwe na amani”.

Aliwashauri viongozi wa kisiasa wawe mstari wa mbele kuhubiri amani na upendo.

Jambo jingine muhimu lililojadiliwa na wachungaji hao ni ugonjwa wa Covid-19.

Wachungaji hao waliwashauri viongozi kupunguza kampeni za mapema kwa sababu mikusanyiko na umati ni hatari na inasababisha kusambaa kwa Covid-19.

“Tunatoa wito wananchi popote walipo wawe makini sana wanapohudhuria mikutano ya wanasiasa kwa sababu inasababisha kuwa na mikusanyiko ya watu wengi kwa pamoja,” alieleza Dkt Ngari.

Alisema jambo muhimu kwa sasa ni wakenya kufuata maagizo ya Wizara ya Afya kwa kuvalia barakoa, kunawa mikono na kuweka nafasi ya angalau mita moja na nusu kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine.

  • Tags

You can share this post!

ONYANGO: Makamishna wa IEBC wasisimamie zaidi ya uchaguzi...

Wanajeshi wawaachilia wafungwa wa kisiasa Guinea