Habari

Wito wadau muhimu wahusishwe katika mpango wa kuunganisha baadhi ya vyuo

July 18th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

BARAZA la Miungano ya Kutetea Haki za Wafanyakazi (TUC-Ke) limeomba wadau wote muhimu washirikishwe katika mjadala wa kuunganisha baadhi ya vyuo vya umma nchini.

Baraza hilo linamtaka Waziri wa Elimu Prof George Magoha kubuni jopo maalumu ambalo litasimamia mchakato wa uunganishi wa vyuo hivyo.

Limesema kuwa kufikia sasa, hakuna uwazi kuhusu utaratibu utakaofuatwa katika mchakato huo.

“Hatupingi kuunganishwa kwa vyuo, lakini lazima pawe na uwazi katika utaratibu utakaofuatwa. Lazima tuige nchi kama Rwanda na Afrika Kusini ambazo ziliweka mikakati thabiti kabla ya kuunganisha vyuo,” amesema Bw Mukhwaya.

Vilevile limepinga mpango wa serikali kuanza kuwaajiri wafanyakazi wake kwa mfumo wa kandarasi.

Nao Muungano wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Nchini (UASU) umetishia kufika mahakamani ikiwa haitashirikishwa kwenye mchakato wa kuunganisha vyuo.

Katibu Mkuu wa UASU, Dkt Constantine Wasonga amesema ni lazima wafafanuliwe kuhusu maana ya mpango huo.

“Tangazo la waziri Magoha ni la kutaka kujizolea sifa tu na halina msingi wowote,” amesema Dkt Wasonga.