Wito wakulima washirikiane na kampuni za pembejeo kuzima wauzaji wa bidhaa ghushi

Wito wakulima washirikiane na kampuni za pembejeo kuzima wauzaji wa bidhaa ghushi

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA wametakiwa kushirikiana na kampuni za pembejeo ili kufanikisha vita dhidi ya mtandao wa wafanyabiashara wanaouza bidhaa ghushi za kilimo.

Kufuatia kukithiri kwa visa vya pembejeo bandia, wakulima wanaendelea kukadiria hasara ya mazao.

Kaunti ya Kiambu, Narok na Uasin Gishu zimetajwa kuongoza katika kero ya uuzaji bidhaa ghushi za kilimo.

“Tunahimiza wakulima kushirikiana na kampuni na mashirika ya pembejeo ili kuzima mtandao wa wafanyabiashara wahuni,” Bw Daniel Mugo, msimamizi wa mauzo eneo la Mlima Kenya wa kampuni ya East Africa Seeds akizungumza jijini Nairobi.

Afisa huyo alisisitiza kwamba ni kupitia ushirikiano wa karibu kati ya wakulima na kampuni changamoto wanazopitia zitaweza kutatuliwa.

Visa vya uuzaji wa mbegu, fatalaiza na dawa bandia na ambazo hazijaafikia ubora wa bidhaa zinaendelea kushuhudiwa.

Matapeli katika soko la zaraa kupitia maduka ya kuuza bidhaa za kilimo, agro vets, wanaendelea kupunja wakulima.

Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa Covid-19 Machi 2020, visa hivyo vimetajwa kuongezeka.

“Mkurupuko wa virusi vya corona ulichangia wakulima kuhadaiwa, wahuni wakapata jukwaa kusakata biashara haramu,” akalalamika Bw Peter Ng’ang’a, mkulima kutoka Kaunti ya Nakuru.

Ng’ang’a hukuza mahindi, maharagwe na pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

“Nimepata hasara ya mahindi misimu kadhaa,” akaelezea, akihimiza serikali na wadau husika katika sekta ya kilimo kukaza kamba oparaseheni kukabili kero ya pembejeo bandia.

Mwaka wa 2016, Muungano wa watengenezaji na wafanyabiashara wa mbegu nchini (STAK) kwa ushirikiano na Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) ilizindua stika yenye kodi zinazotumika kutofautisha mbegu halisi na zile ghushi.

Wateja wakikagua na kununua pembejeo za kampuni ya East Africa Seeds. PICHA | SAMMY WAWERU

Aidha, mwishoni mwa mwaka 2021 wadau hao waliandaa maonyesho ya pembejeo ambapo walihimiza wakulima kutumia stika ya Kephis.

Kando na teknolojia ya STAK na Kephis isiyotoza malipo kutuma ujumbe, East Africa Seeds inasema ina mbinu ya kipekee kufuafitilia bidhaa zake.

“Tuna nambari za siri za vipakio vya bidhaa zetu tunazotumia kufuatilia na kufanya uchunguzi,” Bw Mugo akaambia Akilimali, akiwataka wateja wa kampuni hiyo kuwa huru kuelezea kuhusu sifa za pembejeo zake.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Siasa zimeidunisha na kuteka taaluma ya...

Raia wa Congo taabani zaidi

T L