Habari MsetoSiasa

Wito Washiali ashikwe kwa kushambulia mtu

January 9th, 2020 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

KUNDI la Wakenya linadai kukamatwa na kushtakiwa kwa kiranja wa Bunge la Kitaifa Benjamin Washiali baada ya kumshambulia kijana ambaye hakutambulishwa.

Bw Washiali alionekana kwenye video iliyokuwa ikienezwa mitandaoni akimshambulia kijana huyo kwa mateke na makonde katika barabara inayopitia kwenye shamba la miwa.

Katika kanda hiyo ambayo mbunge huyo alidai ilikuwa ya 2015, anasikika akimshutumu mhasiriwa dhidi ya kuchota mafuta kutoka kwa trekta iliyokuwa ikitumiwa kusafirisha miwa katika Kiwanda cha Sukari cha Mumias.

Video hiyo, ambayo bado haijabainika ni lini ilirekodiwa, imeibua hisia tofauti kutoka kwa wakazi wa Mumias Mashariki na Wakenya mitandaoni.

Kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter, Facebook na makundi ya WhatsApp, Wakenya wanahoji ni kwa nini muundasheria huyo bado yuko huru hata baada ya video hiyo kusambazwa na baadhi ya vyombo vya habari.

“Kitendo hicho hakitarajiwi kutoka kwa mheshimiwa mbunge huyo. Anapaswa kukamatwa kwa kukosa uadilifu,” alisema Bw Edward Shivakali, mkazi wa eneobunge la Mumias Mashariki.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mwakilishi wa Kike Homa Bay Gladys Wanga aliitisha kukamatwa na kushtakiwa mara moja kwa Bw Washiali.

“Tabia iliyodhihirishwa na mbunge huyo haifai kamwe,” aliandika Bi Wanga.

“Tabia hii haiwezi ikavumiliwa. Ni makosa na hairuhusiwi. Anapaswa kuadhibiwa kikamilifu kisheria kwa sababu makosa mawili hayageuki kuwa sawa,” alihoji Bw Bramwel Rotich.

Lakini Bw Washiali ametetea vitendo vyake akisema ni kawaida kwa binadamu wakati mwingine kuwa na tabia tofauti anapokabiliwa na hali fulani.

Alisema hakumjua mwanamme huyo lakini alichukua hatua hiyo kuwalinda wakulima wa miwa na Kiwanda cha Sukuari cha Mumias dhidi ya kupata hasara zaidi.

“Nilipandwa na hasira kutokana na kwamba huku tuking’ang’ana kuimarisha kiwanda, baadhi ya watu waliopania kukisambaratisha walikuwa wakihujumu juhudi zetu,”

“Wakati huo, nilikuwa tu na hiari mbili – kumpeleka kwa polisi ili ashtakiwe na kuharibu maisha yake yote au nimzabe makofi kadha na kumfanya aelewe kwamba alichokuwa akifanya hakikufaa,” alisema.

Mbunge huyo pia alijutia kitendo chake akisema ingekuwa ni wakati huu, hangechukua hatua hiyo.

“Wakati huponya na ni sharti niombe msamaha kwa umma kwa sababu kama kiongozi, singechukua mkondo huo,” alisema