Michezo

Wito wizara itoe mwelekeo kuhusu michezo ya shule

May 8th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUREJELEWA kwa ratiba ya michezo ya shule za upili mwaka huu kutategemea na maamuzi yatakayotolewa na Wizara ya Elimu.

Haya ni kwa mujibu wa David Ngugi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Shule za Upili Nchini (KSSSA), ambaye amefichua mipango ya kukamilisha michuano iliyokuwa ifanyike katika Muhula wa Kwanza iwapo shule zitafunguliwa na masomo ya kawaida kurejelewa kuanzia Juni 4, 2020.

Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za michezo na shule za humu nchini kufungwa kutokana na janga la corona mnamo Machi 2020, michezo ya Muhula wa Kwanza miongoni mwa mwanafunzi ilikuwa ikiendelea katika kiwango cha Kaunti Ndogo.

Shule za Kapsabet Boys na Kapsabet Girls katika Kaunti ya Nandi zilitarajiwa kuwa wenyeji wa michezo ya vikapu, hoki, netiboli, uogeleaji, riadha na raga ya wachezaji saba na 15 kila upande miongoni mwa wanafunzi wa sekondari wakati wa likizo ya Aprili 2020.

Viwanja vya Bukhungu, Mumias Sports Complex na Shule ya Upili ya Kakamega vilikuwa vitumiwe kuandalia mechi za soka miongoni mwa wanafunzi wa kike na kiume.

Ngugi ameshikilia kwamba kurejelewa kwa michezo hiyo ya wanafunzi itafanikisha mipango ya kuandaa mapambano ya makubwa ya pamoja miongoni mwa wanafunzi wa bara zima la Afrika baada ya kufaulu kwa mashindano hayo katika kiwango cha eneo la Afrika Mashariki kwa miaka mingi.

“Tunalenga sasa kutumia michezo kuwaunganisha wanafunzi wote wa bara la Afrika kwa kuwashirikisha katika michezo mbalimbali kila mwaka. Huu ni mpango ambao nina imani utafaulu kutokana na ufanisi ambao tumekuwa tukijivunia katika michezo Jumuiya ya Afrika Mashariki kiasi cha kuwa kivutio ulimwenguni mzima,” akasema Ngugi.

Maamuzi ya kupanua zaidi mashindano ya sasa ya Afrika Mashariki miongoni mwa wanafunzi yaliafikiwa mwaka jana baada ya pendekezo hilo kutolewa na vinara wa Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Shule (ISF) waliokuwa wageni waalikwa katika michezo ya Afrika Mashariki mjini Arusha, Tanzania.

“Waliridhishwa na maandalizi yetu na jinsi michezo hiyo ilivyoendeshwa. Walifurahishwa zaidi na ukubwa wa ushindani miongoni mwa wanafunzi waliowakilisha shule mbalimbali za humu nchini. Hiyo ndiyo sababu iliyotufanya kualikwa kwa Michezo ya Shule Duniani (WSG). Michezo hiyo itaandaliwa China baadaye mwaka huu,” akaongeza Ngugi.