Kimataifa

WIVU: Mama amuua binti aliyependwa zaidi na mumewe

March 21st, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMKE kutoka Ukraine amedaiwa kumuua bintiye wa wiki tatu kwa kumkata shingo, baada ya kuingiwa na wivu kuwa mumewe aligeuka kumpenda mtoto na kupunguza mapenzi dhidi yake.

Mwanamke huyo wa miaka 21 alimuua mwanawe wakati mumewe alikuwa ametoka nje ya nyumba yao katika Jiji la Rivne, Kaskazini Magharibi mwa Ukraine, kwa dakika chache kutupa takataka.

Habari za polisi zimesema kuwa alimvamia malaika huyo punde tu mumewe wa miaka 26 alipotoka na aliporudi alipata mikono ya mkewe ikiwa imejaa damu.

Mwanamume huyo alikimbia chumba cha kulala ambapo mtoto alikuwa amelala na kupata mwili wake ukiwa umelala, huku damu imetapakaa. Akiwa ameshtuka, baba huyo alipiga simu kuitisha msaada.

Maria Momot, mamake mwanamume huyo alieleza Mashirika “Mwanangu alikuwa ametoka kwa dakika chache naye (mkewe) akachukua kisu cha jikoni na kukata shingo ya mtoto.”

Bi Momot alisema mamake mtoto huyo aliingiwa na wivu kwa kudhani kuwa mumewe alikuwa akimpenda, kushinda alivyompenda yeye.

“Mimi na mwanangu tulimpenda mtoto sana. Tulimtunza kadri tulivyoweza. Mkaza mwanangu aliingiwa na wivu kwa kudhani mwanangu alimpenda bintiye kumliko. Leo asubuhi nilimwosha mjukuu wangu na sasa hayuko tena, siamini hili limefanyika katika familia yangu,” akasema.

Waokoaji walipofika wanaripotiwa kumpata mshukiwa akimuuliza mumewe kwanini alikuwa akilia.

Polisi walithibitisha kuwa kilichomuua mtoto huyo ni kukatwa kwa kisu shingoni.

Mshukiwa, hata hivyo, hakueleza sababu ya kutenda uovu huo.

Novemba 2018, mshukiwa alikuwa akiugua ugonjwa wa akili (alipokuwa mja mzito). Ugonjwa huo unaaminika kuathiri afya yake ya akili, ambapo alilazwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili hadi Machi 3, siku chache baada ya kujifungua.

Kwa sasa mwanamke huyo anazuiliwa na polisi, akisubiriwa kufanyiwa uchunguzi wa akili.