Michezo

Wiyeta Girls yazima Bomet Queens 17-0

March 9th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wavulana ya Kapenguria Heroes ilijiweka pazuri kushinda kwa mara ya pili taji la Chapa Dimba na Safaricom katika Mkoa wa Bonde la Ufa msimu huu.

Kikosi hicho kilishinda White Rhino ya Transmara mabao 2-1 kwenye nusu fainali ya kipute hicho cha Chapa Dimba na Safaricom Season Three uwanjani Green Stadium, mjini Kericho. Kwenye nusu fainali ya pili Laiser Hill ilikomoa Tumkas ya Uasin Gishu mabao 2-0.

Kwa wasichana, Wiyeta Girls kutoka Pokot Magharibi ilizima wenzao Bomet Queens ilipowabebesha kapu la magoli 17-0 huku Itigo Girls kutoka Nandi ikichoma Achievers ya Kajiado mabao 6-0.

Kapenguria Heroes ilitangulia kuona lango la wapinzani wao kupitia Alfred Tanui alipotikisa wavu dakika ya 16 kabla ya Tyson Kapchanga kusawazishia White Rhino dakika 17 baadaye. Hata hivyo Kapenguria ilipata bao la ushindi dakika ya 48 kupitia bao lililotupiwa kambani na Wesley Mutai.

Laiser Hill ilitwaa ufanisi huo kupitia Stephene Owino na Timothy Owino waliofunga bao moja kila mmoja dakika ya 43 na 49 mtawalia.

Alex Karani wa Laiser Hill Academy akipiga mpira kumkwepa Kevin Amdavi wa Tumkas kwenye nusu fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three iliyopigiwa Green Stadium, Kericho. Laiser Hill ilishinda mabao 2-0.

”Tumekuwa tukishiriki mazoezi makali tuliandalia fainali za mwaka huu ambapo nashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha mechi safi tena kwa ushindi wa mabao mawili bila jibu,” alisema kocha wa Laiser Hill, Andrew Sango na kuongeza kuwa wanatarajia kubeba ubingwa wa taji hilo msimu huu.

Kikosi cha Itigo Girls kilionyesha mchezo wa kuvutia na kuzoa ushindi huo kupitia Marion Wafula aliyepachika wavuni mabao manne kunako dakika ya 12, 25,60 na 86. Naye Claudia Kadenge alifumwa mabao mawili dakika ya 18 na 47.

Nayo Wiyeta Girls ilibugiza wapinzani wao kupitia Opisa Shaylene aliyecheka na wavu mara sita kunako dakika ya 16, 23, 77, 79, 81 na 90. Naye Aujat Dorine aliifungia mabao manne dakika ya 9,13, 46, 57 na 77, 79, 81 na 90 mtawalia.

Aidha Wanda Edina aliitingia mabao matatu huku Musiliri Diana akitupia kambani mabao mawili. Katika fainali wavulana wa Kapenguria Heroes walitazamiwa kukabili Laiser Hill nacho kikosi cha Wiyeta Girls kilipangwa kuchuana na Itigo Girls.

Mabingwa wa taji hilo, kitengo cha wavulana na wasichana watajikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ambazo zimepangwa kuandaliwa mjini Mombasa Mwezi Juni mwaka huu.

Alfred Tanui wa Kapenguria Heroes (kushoto) akishindana na John Williams wa White Rhino kwenye nusu fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three iliyopigiwa Green Stadium, Kericho. Kapenguria Heroes ilishinda mabao 2-1. 

Kando na hayo, timu hizo mbili kila moja itapokea kitaita cha Sh200,000. Nazo timu zitakaomaliza katika nafasi mbili kila moja itapoongezwa kwa Sh100,000.

Washindi wa eneo hilo watajiunga na wenzao kutoka maeneo mengine kufuzu kwa fainali za kitaifa. Wavulana watajiunga na wenzao wa Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati , Dagoretti Mixed (Mkoa wa Nairobi),

Tumaini School (Mkoa wa Mashariki)na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa. Wasichana watajiunga na Falling Waters Mkoa wa Kati, Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.