Michezo

Wiyeta na Laiser Hill mabingwa wa Chapa Dimba Bonde la Ufa

March 10th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Wiyeta Girls kutoka Pokot Magharibi ilirejea kwa kishindo ambapo ilitawazwa malkia katika Mkoa wa Bonde la ufa, kwenye mechi za Chapa Dimba na Safaricom Season Three muhula huu.

Katika fainali zilizopigiwa uwanjani Green Stadium, mjini Kericho, Wiyeta Girls ilitawazwa mabingwa baada ya kunyamazisha Itigo Girls kutoka Nandi kwa mabao 3-0.

Kitengo cha wavulana Laiser Hill Academy kutoka Kajiado ilibeba taji hilo ilipochoma Kapenguria Heroes mabao 4-2 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida.

Chipukizi wa Wiyeta walipata bao la kwanza kupitia juhudi zake Edina Wanda dakika ya 11 kabla Jacinta Karemana na Opisa Shaylene kutikisha wavu mara moja kila mmoja kunako dakika ya 34 na 45 mtawalia.

Katika fainali ya wavulana matumani ya Kapengeria Heroes kushinda ubingwa huo kwa mara ya pili yaliambulia patupu walipozidiwa maarifa na wapinzani wao kwa mipigo ya matuta. Katika muda wa kawaida Samson Tanui alifungia Laiser nayo Kapenguria ilisawazisha kupitia Majabe Shariff.

”Nashukuru chipukizi wangu kwa kufuata mawaidha ipasavyo na kumakinika vilivyo dimbani ambapo juhudi zao hatimaye zilizaa matunda ya kuibuka mabingwa wa eneo hili,” alisema kocha wa Laiser Hill, John Mwaura na kuongeza kuwa hii ndio iliyokuwa mara ya pili kushiriki ngarambe hiyo.

NUSU FAINALI

Kwenye nusu fainali, Wiyeta Girls ilizima Bomet Queens kwa kuikandamiza kwa magoli 17-0 huku Itigo Girls ikirarua Achievers ya Kajiado mabao 6-0.

Kapenguria Heroes iliilemea White Rhino ya Transmara kwa mabao 2-1 nao wanasoka wa Laiser Hill Academy walitia kapuni tiketi ya kushiriki fainali walipocharaza Tumkas ya Uasin Gishu mabao 2-0 yaliyofungwa kupitia Stephene Owino na Timothy Owino waliotinga bao moja kila mmoja.

Mabingwa hao (wavulana na wasichana) kila moja ilituwa Sh200,000 na kujikatia tiketi za kufuzu kushiriki fainali za kitaifa zitakaoandaliwa mjini Mombasa mwezi Juni mwaka huu. Nazo Kapenguria Heroes na Itigo Girls zilizomaliza katika nafasi ya pili kila ilipongezwa kwa Sh100,000.

Kwenye fainali za kitaifa mabingwa wa kipute hicho hutuzwa Sh1 milioni kitengo cha wavulana na wasichana.

TUZO

Diana Musiliri (Wiyeta Girls) na Timothy Ouma (Laiser Hill) waliibuka wachezaji wanaoimarika ka wasichana na wavulana mtawalia. Kwa wafungaji bora, Opisa Shaylene wa Wiyeta aliibuka shujaa alipoitingia mabao saba kwa wasichana naye Alfred Tanui aliifungia Kapenguria heroes mabao mawili.

Tuzo ya wanyakaji Muimi James wa Laiser Hill na Emelda Ingaitsa wa Wiyeta girls walituzwa walinda lango bora mwaka huu.

Wavulana hao Laiser Hill (Mkoa wa Bonde la Ufa) wamejiunga na wenzao kutoka maeneo mengine ikiwamo Berlin FC (Mkoa Kaskazini Mashariki), Ulinzi Youth (Mkoa wa Kati), Dagoretti Mixed (Mkoa wa Nairobi), Tumaini School (Mkoa wa Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.

Kitengo cha wasichana, Wiyeta Girls (Mkoa wa Bonde la Ufa) wamenasa tiketi ya fainali pamoja na Falling Waters Mkoa wa Kati, Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.

Alfred Tanui wa Kapenguria Heroes (kushoto) akishindana na John Williams wa White Rhino kwenye nusu fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three iliyopigiwa Green Stadium, Kericho. Kapenguria Heroes ilishinda mabao 2-1. Picha zote/ John Kimwere