Makala

Wiyoni yaipa Lamu usasa mtamu

April 25th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

MARA nyingi kisiwa cha Lamu kila kinapotajwa, taswira inayojichora kwa fikra za wengi ni historia, ukale, na majumba ya magofumagofu.

Yote hayo yanatokana na kwamba kitovu cha kisiwa hicho ni Mji wa Kale wa Lamu ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 700.

Mji huo wa kale unavuma kwa historia yake ya kipekee na jinsi ambavyo wakazi wa hapa, ambao wengi ni wa jamii ya Waswahili wa asili ya Kibajuni, wamejizatiti kuhifadhi utamaduni, desturi na ukale wao wa karne na karne.

Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliorodhesha Mji wa Kale wa Lamu kuwa miongoni mwa sehemu zitambulikazo zaidi duniani kwa kuhifadhi tamaduni na ukale, yaani Unesco World Heritage Site.

Hatua hiyo ilizidi kugandisha fikra za waja wengi kuhusu Lamu kwamba ni eneo ambalo mambo yake ni ya kizamanizamani na yaliyopitwa na wakati.

Ila wasichokijua ni kuwa eneo hilo pia lina mitaa au sehemu ambazo usasa umesheheni. Mojawapo ya maeneo hayo ya kisiwa cha Lamu ni Wiyoni.

Miaka ya hivi karibuni, Wiyoni limechipuka kuwa eneo lenye majumba ya kisasa na ya kifahari, hivyo kubandikwa jina ‘Dubai Ndogo’ kutokana na linavyoipa Lamu sura ya usasa.

Kwa kawaida, majumba mengi yanayojengwa kwenye Mji wa Kale wa Lamu hufuata mfumo mmoja, hasa ule wa nchi ya Oman, ambapo nyumba hujengwa katika ramani au muonekano unaoshabihiana na ule wa misikiti.

Msikiti uliojengwa na kukamilika hivi majuzi katika eneo la Wiyoni. Maendeleo ya eneo hilo yameipa Lamu usasa mtamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ila katika eneo la Wiyoni, mambo ni tofauti. Hapa, utapata nyumba nyingi za kisasa na maghorofa marefumarefu, yakiwa yamesheheni na ambayo yamejengwa kwa muundo wa kisasa.

Wiyoni ni eneo ambalo liko takriban kilomita moja kutoka Mji wa Kale wa Lamu, japo pia liko ndani ya kisiwa hicho hicho cha Lamu.

Wamiliki wa majumba Wiyoni wamekuwa wakifurahia uhuru wa kujijengea nyumba zao bila vizuizi vyovyote vya ni ramani ipi wanayofaa kufuata.

Hicho ni kinyume kabisa na wenzao walioko kwenye Mji wa Kale wa Lamu, ambalo ni eneo la kihistoria, ambapo hawawezi kuendeleza ujenzi wowote bila kufuata kanuni au ramani zifaazo au zinazokubalika.

Bw Abdalla Omar, mmoja wa wamiliki wa nyumba za kisasa mtaani Wiyoni, anasema angalau wapangaji wanaoishi kisiwani Lamu wanafursa ya kujichagulia pa kuishi kinyume na wali.

“Zamani watu walihisi kukandamizwa kuishi sehemu wanakojihisi kuwa mambo yake ni ya zamanizamani kama katikati ya Mji wa Kale wa Lamu. Leo hii wengi wanakimbilia kuishi Wiyoni, wakijua fika kuwa eneo hili linadhihirisha au kuwakilisha vyema usasa,” akasema Bw Omar.

Mohamed Kombo, mkazi wa Mji wa Kale wa Lamu, anakiri kuwa maendeleo yanayoshuhudiwa Wiyoni miaka ya hivi karibuni yastahili kupigiwa upatu.

Anasema kinyume na mjini Lamu ambapo nyumba zimeshikanashikana, hivyo kuzidi kuleta sura ya zamani, mpangilio wa majumba Wiyoni umepeana nafasi nzuri, hivyo kuleta muonekano wa kuridhisha.

“Wacha kweli ile sehemu iitwe Dubai Ndogo. Imepiga hatua kubwa kimaendeleo. Ukifika Wiyoni utajihisi kana kwamba kweli upo Dubai na si kisiwani Lamu. Kuna majengo mapyamapya na yaliyowekwa katika mpangilio bora wenye kuleta muonekano halisi wa kisasa,” akasema Bw Kombo.

Lakini je, wajua Wiyoni ilianza vipi?

Kulingana na wazee, sehemu nyingi za Wiyoni ambazo kwa sasa ni nchi kavu au ardhi zilikuwa ndani ya maji au Bahari Hindi.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee na Mwanahistoria wa Lamu, Mohamed Mbwana Shee, anasema miaka ya tisini (1990s), wakati kulipotekelezwa shughuli ya kuchimba na kuongeza kina cha maji ya kivuko cha Mkanda kilichoko karibu na Wiyoni, kifusi kilichotolewa kilibebwa na kumiminwa kwenye fuo za Bahari eneo hilo.

Uchimbaji huo ulitekelezwa ili kuwezesha boti, mashua, jahazi na vyombo vingine vikubwavikubwa kupita eneo hilo la kivuko cha Mkanda ambalo kina chake kilikuwa kifupi.

Sehemu mojawapo yenye majumba ya kisasa katika eneo la Wiyoni, kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mbwana anasema ni kutokana na hali hiyo ambapo maji ya Bahari yalianza kuhama polepole kwenye fukwe za Wiyoni hadi kuacha sehemu kubwa ya ardhi kavu ipatikanayo sasa.

“Kwanza sehemu ya Wiyoni haikumilikiwa na yeyote. Ilikuwa ardhi ya umma. Baada ya kifusi kumwagwa na ardhi kubwa kupatikana, hapo ndipo watu walipoanza kung’ang’ania umiliki wa ardhi eneo hilo,” akasema Bw Mbwana.

Bw Mbwana alifichua kwamba mmoja wa viongozi wa kisiasa waliowahi kuhudumu Lamu ndiye aliyevamia eneo hilo la Wiyoni, ambapo aliweka seng’enge kulizingira, hivyo kulibinafsisha.

“Diwani mmoja aliyehudumu kisiwani hapa ndiye aliyetumia njia za kijanja kumiliki ardhi ya Wiyoni. Baadaye aliikatakata vipandevipande na kuiuzia watu. Hiyo ndiyo sababu utapata wamiliki tofautitofauti wa ardhi eneo hilo la Wiyoni leo. Kila mmoja yuko mbioni kuendeleza ardhi yake kama inavyoshuhudiwa,” akasema Bw Mbwana.

Mbali na nyumba za kupangisha na zile za makazi (kuishi), pia utapata hoteli za kifahari zilizojengwa Wiyoni ambazo tayari zimeanza kuvutia wageni na watalii, sawa na inavyoshuhudiwa kwenye mji wa kale wa Lamu.

Kisiwa cha Lamu, ambacho kinajumuisha maeneo ya Wiyoni, Shela, Kipungani, Matondoni, Makafuni, Kashmiri, Kandahar, Bombay, India, Hidabo na viunga vyake ni makazi ya zaidi ya watu 30,000.