Habari Mseto

Wizara ya Afya yafundisha Wakenya jinsi ya kuvalia barakoa

April 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WIZARA ya Afya imeonekana kugundua Wakenya wengi hawajui kuvalia barakoa baada ya kuanza kuwahamasisha jinsi ya kuzivalia ili kuzuia maambukizi wakati huu wa janga la virusi hatari vya corona.

Kupitia mtandao wake wa kijamii hapo Alhamisi, wizara hiyo imeonyesha makosa mengi, ambayo Wakenya wanafanya na kufanya vita dhidi ya virusi hivyo kuwa kazi bure.

Kosa la kwanza ni kuwa Wakenya wamekuwa wakifanya ni kuvalia barakoa kufunika kinywa pekee. Pili, kuvalia barakoa kwenye kipaji. Tatu, mtu kuvalia barakoa kwenye kidevu. Kuvalia barakoa kwa kufunga kamba zake zikipitana pia ni kosa.

Kuvalia barakoa vizuri, wizara hiyo inasema, kutasaidia kukomesha uenezaji ya ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Hapo Jumatano, Shirika la Amref Health Africa pia lilisema kuvalia barakoa chafu, kuacha kamba zikining’inia ama kunining’iniza barakoa kwa kutumia kamba moja pamoja na kuachilia nywele kando ya uso ni makosa.

Mwandishi huyu pia ameshuhudia Wakenya wengi wakibeba barakoa mkononi badala ya kuzivalia.

Njia nzuri ya kuvalia barakoa ni kuhakikisha inafunika kinywa na pua. Hakikisha nywele zinalala mgongoni. Funga kamba za barakoa nyuma ya kichwa na shingo bila ya kuzipitanisha. Unapotaka kuvua barakoa, itoe kutokea nyuma ya kichwa.

Kufikia Aprili 23, Kenya ilikuwa imeripoti visa 320 baada ya watu 17 kupatikana na virusi hivyo katika saa 24 zilizopita. Virusi hivyo vimeua watu 14 nchini Kenya na 185, 461 duniani.