Habari Mseto

Wizara ya Elimu yaishangaa NLC kununua ardhi bila hatimiliki

May 17th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WIZARA ya Elimu imeshutumu Tume ya Ardhi nchini (NLC) kwa kutumia Sh1.5 bilioni kununua ardhi ya shule mbili za umma, bila hati za umiliki.

Tume hiyo inasemekana kununua vipande hivyo katika eneo la Ruaraka, Nairobi.

Katibu Mkuu wa Elimu Dkt Belio Kipsang wakati wa mahojiano mbele ya kamati ya seneti alisema licha ya kuandikia barua tume hiyo kupata hatimiliki ya ardhi kutoka Kampuni ya Afrison Import and Export Limited, tume hiyo ilikiuka ombi hilo.

Maseneta hao walikuwa wakihoji Dkt Kipsang kuhusiana na utwaaji wa lazima wa ekari 13.534 ambamo shule ya upili ya Ruaraka na Shule ya Msingi ya Drive zimejengwa kwa jumla ya Sh3.2 bilioni.

Wizara hiyo kupitia kwa NLC ililipa Sh1.5 bilioni kwa shamba la Whispering Farms Limited. Shule hizo mbili zilijengwa miaka 34 na 32 iliyopita kwa shamba la kibinafsi.