Habari MsetoSiasa

Wizara ya Matiang'i inaongoza kwa ufisadi – EACC

November 19th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WIZARA ya Usalama wa Ndani ndiyo fisadi zaidi nchini, utafiti wa hivi punde wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) umeonyesha.

Tume hiyo iliyotolewa Jumanne iliorodhesha idara tatu zilizo chini ya wizara hiyo kama zilizokithiri ufisadi zaidi.

Ripoti hiyo inasema kwamba wizara hiyo inayosimamiwa na Dkt Fred Matiang’i inaongoza kwa asilimia 47.5 ya visa vya ufisadi ikifuatwa na wizara ya Afya ya waziri Sicily Kariuki ikiwa na asilimia 17.9 ya visa vya ufisadi na wizara ya kilimo inayosimamiwa na Mwangi Kiunjuri ikiwa na asilimia 13.8 ya visa vya ufisadi.

Visa vya ufisadi katika Wizara ya Ardhi ya waziri Farida Karoney vilipungua kutoka asilimia 23.9 mwaka wa 2017 hadi 11.0 mwaka jana.

Kulingana na ripoti ya hivi punde, idara usajili za watu, huduma ya polisi na machifu zinaongoza kwa ufisadi nchini.

Idara ya usajili wa watu inahusika na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo nchini.

Ripoti hiyo ilisema asilimia 19.9 ya visa vya ufisadi viliripotiwa katika idara ya usajili wa watu na asilimia 19.7 katika hospitali za umma.

Kwenye utafiti huo uliofanywa 2018, machifu walitajwa kuhusika na asilimia 16 ya visa vya ufisadi nchini. Machifu pia wako chini ya wizara ya usalama wa ndani.

Mwenyekiti wa EACC Askofu Eliud Wabukhala alisema hii ilikuwa mara ya kwanza Kenya kurekodi kiwango cha chini cha ufisadi tangu 2012.

“Kiwango cha wastani ya hongo kilishuka kutoka Sh 5,058.75 miaka miwili iliyopita hadi Sh 3,833.14 mwaka jana,” alisema Bw Wabukhala.

Maafisa wa polisi walichangia asilimia 39 ya visa vya ufisadi ikifuatwa na Kenya Power iliyosajili asilimia 12 ya visa vya ufisadi huku Bima ya Taifa ya Afya ikirekodi asilimia 11 ya visa vya ufisadi mwaka jana.

Walioshirikishwa kwenye utafiti huo walisema ufisadi ndio changamoto kuu inayokabili Kenya kwa wakati huu na kwamba wanaamini wanahabari wanafanya kazi nzuri kupiga vita ufisadi.

Changamoto nyingine ambayo waliohusishwa walitaja inayokabili Kenya ni ukosefu wa ajira (asilimia 36.8), umasikini na ukame (asilimia 27.2) na gharama ya maisha (asilimia 16.9).

Akitoa ripoti hiyo jana, Bw Wabukhala aliwataka maafisa wa serikali wanaohusishwa na ufisadi kujiuzulu hadi kesi zinazowakabili zisikilizwe na kuamuliwa.