Michezo

Wizara yafuatilia shughuli za ujenzi wa uwanja wa kisasa Mombasa

May 30th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WAPENZI wa mchezo wa mpira wa miguu Mombasa na sehemu nyinginezo za mwambao wa Pwani wana matumaini uwanja wao wa Kaunti ya Mombasa kuendelea kujengwa.

Mashabiki wa sehemu hiyo wanaweza kuwa na matumaini ya kushuhudia mechi kubwa za kimataifa kutokana na Wizara ya Michezo kuamua kufuatilia shughuli za ujenzi wa uwanja wa kisasa Mombasa.

Hayo ni kulingana na Waziri wa Michezo na Utamaduni, Balozi Amina Mohamed aliyesema ujumbe wa wizara yake unatarajia kutembelea uwanja huo kipindi cha wiki mbili zijazo kushuhudia jinsi ujenzi wake unavyoendelea.

“Ujumbe wa wizara yetu utafika Mombasa kushuhudia kama kazi za ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Mombasa zinaendelea na kujua mahitaji yanayohitajika uwanja huo ukamilike kwa haraka ili vijana wa Pwani wapate kuutumia kuinua vipaji vyao,” akasema Amina.

Balozi Amina anasema wizara yake inataka kutimiza ahadi zote zilizotolewa na Rais Uhuru Kenyatta kwa kuhakikisha kunajengwa viwanja vya kisasa katika sehemu mbalimbali nchini.

“Kwa wakati huu, tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha viwanja vya Nyayo, Kasarani jijini Nairobi na Kipchoge Keino wa mjini Eldoret vimemalizika kufikia Januari mwakani na kuanza kutumiwa kwa mashindano na mechi za kitaifa na kimataifa,” akasema.

Amina anasema Idara ya Michezo ya wizara yake imeweka maafisa wake kwenye kila shirikisho la michezo kwa ajili ya kusaidia kutatua matatizo yanayokabili yanayokabili michezo mbalimbali.

Amesema maafisa hao huwa wanasaidia kutoa mashauri ya jinsi ya kufanikisha mipango yao ya kushirikisha timu zao kwenye mashindano na michezo ya kimataifa na pia kujulisha wizara fedha za kugharamia safari za timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

“Mbali na kuwa na wawakilishi wetu kwenye mashirikisho ya michezo mbalimbali, huwa tuna maafisa maalum ambao wanakuwako kwenye Baraza la Michezo la Kenya (KNSC), Kenya National Olympic Committee (NOCK) na Kamati ya Olimpiki ya Walemavu,” akasema.

Balozi Amina anasema ushirikiano wa wizara hiyo na mashirikisho ya michezo yapatayo 60 yakiwemo yale ya soka, riadha na raga na mengineyo ni mzuri kwani wanafanya kazi pamoja kwa ajili ya kuipatia sifa na kuitangaza nchi ya Kenya huko ng’ambo.

“Tunaamini ni ushirikiano na kufanya kazi pamoja ndiyo yatakayowezesha michezo yetu kupiga hatua ya maendeleo. Pia tunahakikisha mashirikisho hayo yanafuata sheria za msajili wa michezo,” akasema.

Waziri Amina aliwaomba wachezaji pamoja na wakufunzi wao wajitayarishe kwa mazoezi ili mara baada ya janga la corona kumalizika ama ruhusa ya kucheza kutangazwa, wawe wako tayari kuwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa.

Waziri wa Michezo na Turathi Amina Mohamed (kati) akiwa na maafisa wake wakizuru eneo mojawapo la miradi ya michezo. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Alisema serikali inajivunia kuwa wana michezo wote wanaoiletea sifa nchi na ndio maana wizara yake inajitolea kuzisaidia timu za michezo mbalimbali zinazokwenda ng’ambo kwa mashindano ya kimataifa.

“Tunajitahidi kuzisaidia timu zinazojiandaa kwa mazoezi ya mashindano ya kimataifa na nyakati za mashindano hayo kwa kuzipatia fedha zinazotoka kwenye Hazina ya Michezo,” akasema Amina.

Alisifu timu kadhaa zilizofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa na kuutaja mchezo wa Tong-IL Moo-Do kuwa miongoni mwa michezo ambayo iliipatia sifa kubwa Kenya ilipomaliza nafasi ya pili kwenye Mashindano ya Dunia yaliyofanyika nchini Korea Kusini.

“Mbali na kumaliza nafasi ya pili kwenye mashindano hayo ya dunia, timu ya Kenya kwa jina maarufu la Jasiri ilifanikiwa kuhifadhi taji lake la Mombasa Open kwa mwaka wa saba mfululizo, hivyo kutufanya tujivunie,” akasema.

Amina alisema wanashirikiana vizuri na maafisa wa shirikisho la Tong-IL Moo Do katika juhudi za kuufanya mchezo huo ufikie kiwango na umaarufu sawa na michezo mingine ambayo inailetea Kenya sifa.

“Naamini viongozi wa michezo yote watashirikiana na wizara yangu katika kuinua hali ya michezo hasa kwa vijana ambao wanahitajika washiriki michezo badala ya kujiingiza kwenye vitendo vibaya ambavyo vinaweza kuangamiza maisha yao,” akasema Balozi Amina.