Wizara yamtishia mwalimu aliyefichua masaibu yake

Wizara yamtishia mwalimu aliyefichua masaibu yake

Na WYCLIFFE NYABERI

WAKUU wa elimu katika Kaunti ya Narok, wametishia kumwadhibu mwalimu kwa kuwafichulia wanahabari matatizo yanayokumba shule yake.

Kwenye toleo la jana, Taifa Leo iliangazia masaibu anayopitia mwalimu mkuu wa shule ya kutwa ya upili ya Sosiana, Bi Magdalene Njoki Kimani, pamoja na maafisa wanaosimamia mtihani wa kitaifa (KCSE), kwa kutembea zaidi ya kilomita 20 kila siku kuwapelekea watahiniwa karatasi za mtihani.

Sababu za kutembea kwao ni kutokana na hali mbovu ya barabara inayounganisha shule hiyo.

Maafisa hao hutembea kilomita 10 asubuhi wakipeleka karatasi za maswali, na kiasi sawia na hicho wanaporudisha karatasi za majibu. Kisha huwa wanachukuliwa na gari linalowabeba kuelekea mji wa Emurua Dikirr, ambako ndiko kuliko na kontena ya kuhifadhi mtihani wa shule za eneo hilo.

Mkurugenzi wa elimu katika Kaunti Ndogo ya Transmara Mashariki, Bw Steve Gachie alimwagiza mwalimu huyo afike afisini mwao kuandikisha taarifa kuhusu kwa nini alikubali kuhojiwa na wanahabari.

“Ni nani aliyewaambia kilomita anazozitembea ni 20? Mbona aongee ilhali ni Wizara ya Elimu inayofaa kuulizwa maswali kama hayo?” Bw Gachie akagombana jana.

Mkurugenzi huyo hakukomea hapo, kwani aliendelea kulalama na kudai kwamba amechafuliwa jina kupitia kwa makala hayo.

Kulingana naye, umbali ambao walimu na maafisa wanaosimamia KCSE shuleni humo hutembea ni kilomita tisa.

“Ni barabara ngapi za Transmara ambazo hazipitiki? Mbona mnachapisha habari kama hizi zilizofanya niulizwe maswali chungu nzima?” akalalama Bw Gachie kwenye simu.

Alipuuzilia mbali wanaomtaja mwalimu huyo kuwa jasiri anayefaa kutunukiwa.

You can share this post!

Corona: Hitilafu ya oksijeni hospitalini yaua watatu

Msomi akiri kukiuka maadili kwenye mahojiano ya Jaji Mkuu