Habari Mseto

Wizara yasaka Sh6 bilioni kukabili njaa

March 16th, 2019 2 min read

Na IBRAHIM ORUKO

WIZARA ya Ugatuzi inaomba Wizara ya Fedha Sh6 bilioni ambazo itatumia kukabili baa la njaa linalotarajiwa kukumba kaunti 14 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Waziri Msaidizi wa wizara hiyo (CAS), Hussein Dhadho alisema kuwa wizara yake tayari imetuma maombi kwa wizara ya Fedha, ili njaa isigeuke janga nchini.

“Makadirio yetu ni kuwa tunahitaji kati ya Sh6 bilioni na Sh8 bilioni kukabili njaa ambayo inatokana na kiangazi kilichoko. Tumewasilisha ripoti kwa Wizara ya Fedha na tunatumai kuwa itashughulikiwa haraka,” Bw Dhadho alisema.

Mamlaka ya Kitaifa ya Kushughulikia Ukame imesema kuwa watu 800,000 katika kaunti 23 wanakumbwa na kiangazi.

Kaunti kame tayari zimeonywa kujiandaa kwa uhaba wa chakula, maji na lishe ya mifugo wiki chache zijazo. Mamlaka hiyo imetahadharisha kaunti saba kujiandaa kwa kiangazi.

Bw Dhadho aliyefika mbele ya kamati ya seneti kuhusu Ugatuzi, alisema tayari njaa imesababisha vifo vya watu wawili Kaunti ya Turkana.

Mwenyekiti wa kamati hiyo John Kinyua alionya kuwa vifo vinavyotokana na njaa havitaruhusiwa, akiitaka serikali kuharakisha kuokoa maisha ya watu.

“Tunataka kuona serikali ikishughulikia suala hili kwa njia ifaayo. Vifo vinavyotokana na njaa haviruhusiwi,” akasema Bw Kinyua.

Bw Dhado alisema serikali inachukulia suala hilo kwa uzito, na kuwa wizara yake inasubiri kupokea pesa kutoka kwa wizara ya Fedha tu.

“Tayari tunazungumza na wahisani kusaidia katika hali hii,” alisema.

Kiangazi

Baadhi ya kaunti ambazo hali yake ya kiangazi imekuwa ikiharibika ni Kitui, Turkana, Marsabit, Samburu na Tana River.
Nyingine ni Garissa, Tharaka, Mandera, Wajir, Pokot Magharibi, Meru (Kaskazini) na Kilifi.

Kaunti za Isiolo, Laikipia, Taita Taveta, Lamu, Embu, Kajiado, Baringo, Makueni, Nyeri (Kieni) na Narok ziko katika hali nzuri.

“Hali hii ya kiangazi imesababishwa na kupungua kwa mvua ambayo ilishuhudiwa Desemba,” ripoti inasema.

Ijapokuwa idara ya utabiri wa hali ya hewa ilikuwa imetabiri kuwa nchi ingepata mvua ya kutosha mwishoni mwa mwaka jana, kipindi cha Oktoba-Desemba hakikuwa na mvua ya kutosha, na ilinyesha katika maeneo machache.

Mamlaka hiyo inasema kuwa hali imeendelea kuwa mbaya tangu Novemba mwaka jana ambapo ni kaunti tatu zilizokuwa na uhaba wa chakula.