Habari

Wizara yasitisha kwa muda uteuzi wa wanaolenga kusomea kozi ya ualimu P1

September 19th, 2019 1 min read

Na OUMA WANZALA

WIZARA ya Elimu imesitisha kusajili wanaotaka kusomea taaluma ya ualimu wa shule ya msingi, kategoria ya P1 ili kuipa Taasisi ya Kuunda Mitaala (KICD) muda kulainisha masomo kuafiki mfumo mpya unaojikita katika umilisi (CBC).

Agizo la wizara limeanza kutekelezwa mwezi huu wa Septemba.

Hata hivyo, Katibu katika wizara, Belio Kipsang amesema usajili katika vyuo vitatu vinavyotoa mafunzo ya stashahada kwa wanafunzi wa ualimu vitaendelea na shughuli ambapo masomo yanatarajiwa Januari mwakani.

“Uteuzi wa kusajili watakaosomea ualimu kiwango hicho cha diploma ambao hufanywa na Huduma ya Uteuzi wa Wanafunzi katika Vyuo Vikuu na Vyuo (KUCCPS) utaendelea,” amesema Dkt Kipsang.

Kwa miaka kadhaa, serikali imekuwa ikiwateua wanafunzi wa kusomea kozi ya ualimu wa shule za msingi na chekechea – ECDE na P1 – kuanzia Aprili kila mwaka kilele kikiwa na waliofaulu kujiunga na vyuo husika Septemba.

Dkt Kipsang amesema wizara iko mbioni kuhakikisha shule na taasisi zote muhimu zinafaulisha mfumo mpya wa elimu unaoweka zingatio kwa umilisi.

Ameongeza kwamba KICD inataka kuja na mkakati wa ufundishaji wa walimu.

“Hii ndiyo sababu wizara iliamua kusitisha usajili wa wanafunzi wa kusomea kozi za ualimu wa chekechea na shule za msingi mwaka 2019. Vyuo vya kutoa mafunzo ya kozi za ualimu vinatakiwa kujiandaa usajili wa hatua ya diploma ambapo masomo yataanza Septemba 2020,” amesema Kipsang kwenye tangazo maalumu lililotumiwa wakurugenzi katika maeneo mbalimbali na wakurugenzi wa elimu katika kaunti kote nchini.

Vyuo hivyo vilikuwa vikisajili idadi ya wanafunzi 20,000 kila mwaka huku vyuo binafsi vikiwa na nafasi za wanafunzi 4,000.

Jana Jumatano wanafunzi wa gredi ya tatu walifanyiwa tathmini ya mfumo huo wa CBC.