Wizara yataka Wakenya waliopoteza ajira walipwe na serikali

Wizara yataka Wakenya waliopoteza ajira walipwe na serikali

Na SAMWEL OWINO

WIZARA ya Leba inataka sehemu ya mkopo wa Sh257 bilioni ambazo Kenya ilipata kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF), kuelekezwa katika wizara hiyo ili kuwasaidia wafanyakazi ambao wamepoteza ajira.

Wizara hiyo ilisema itawasaidia wafanyakazi waliopoteza kazi zao katika kaunti za Nairobi, Nakuru, Machakos, Kiambu na Kajiado, baada ya kufungwa na serikali ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Hapo jana, Waziri wa Leba, Simon Chelugui aliliambia Bunge la Kitaifa kwamba wanajadiliana na Wizara ya Fedha kuhusu kiasi cha fedha itakachotengewa ili kuwasaidia wafanyakazi hao.

Kwenye kikao kilichoandaliwa kwa njia ya mtandao, Bw Chelugui aliwaambia wabunge kuwa wizara hiyo iko kwenye hatua za mwisho kukusanya idadi kamili ya wafanyakazi waliopoteza ajira zao kabla ya kuwasilisha maelezo hayo kwa Wizara ya Fedha.

Kikao hicho kiliandaliwa kujadili hatua zilizochukuliwa kuwasaidia Wakenya kuhimili athari za janga la virusi vya corona.

“Tunafanya juhudi kuona kuwa wizara yetu imetengewa sehemu ya mkopo wa IMF. Siwezi kueleza kiwango halisi tunachotaka kwani maafisa wetu bado wanaendelea na taratibu za kutathmini fedha tunazohitaji ili kuwasaidia wenyeji wa kaunti tano zilizoathiriwa na hatua hizo. Kaunti ambazo zinapakana na maeneo hayo pia zitajumuishwa kwenye mpango huo,” akasema Bw Chelugui.

Waziri alieleza masikitiko kwamba wafanyakazi wengi ambao walikuwa wakiendelea na shughuli zao katika maeneo mbalimbali sasa hawana ajira kutokana na kufungwa kwa maeneo hayo.

Alionya huenda watu kama hao wakajihusisha kwenye maovu kama wizi kama njia ya kujipatia riziki.

“Kuna watu ambao walikuwa wakifanya kazi na kujipatia riziki. Hata hivyo, maeneo hayo yalifungwa. Kutokana na hatua hizo, sasa tuna watu ambao ni maskini, hali ambayo huenda ikazua mzozo katika jamii. Huenda wakaanza kujihusisha katika vitendo kama uhalifu. Hivyo, tunataka kubuni mikakati ya kuwasaidia kukabiliana na athari za kiuchumi,” akasema.

Katibu katika wizara hiyo, Bw Peter Tum, pia aliwaambia wabunge kuwa wimbi la tatu la maambukizi limewapotezea watu wengi ajira zao lakini wanafanya kila wawezalo kudhibiti hali hiyo.

You can share this post!

Jaji Mkuu: Uamuzi wa usiku watatiza Koome

‘Uhuru na Raila wanataka kura ya maamuzi upesi’