Habari za Kitaifa

Wizara yatoa taarifa kufuatia ajali iliyohusisha wanafunzi wa Kapsabet Boys

March 16th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI mnamo Jumamosi ilisema kuwa zaidi ya wanafunzi 10 wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapsabet waliohusika katika ajali iliyotokea katika barabara ya Kabarnet-Marigat, wamehamishiwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), mjini Eldoret.

Ajali hiyo ilifanyika katika eneo la Patkawanin kwenye barabara hiyo.

Kulingana na Katibu wa Elimu Belio Kipsang’, serikali  ilichukua hatua hiyo ili kuhakikisha wanafunzi hao wanapata matibabu maalum.

Kwenye ajali hiyo iliyofanyika mwendo wa saa saba za mchana Jumamosi, watu wawili—mwanafunzi na mwalimu—waliaga dunia.

Basi hilo lilianguka na kubingiria mara kadhaa baada ya kukumbwa na matatizo ya kimitambo.

Wanafunzi hao zaidi ya 216 ni wa Kidato cha Pili walikuwa wakielekea kwa ziara ya kimamoso katika Ziwa Bogoria, lililo katika eneo la Baringo Kusini.

Walijumuisha walimu sita na walikuwa wakisafiria mabasi manne.

Katibu huyo, aliyezuru Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Baringo, ambako baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa walikuwa wamelazwa, alisema wanafunzi 51 watabaki katika hospitali hiyo ili hali zao ziweze kufuatiliwa na madaktari.

Wanafunzi wengine waliokuwa katika mabasi matatu yaliyobaki wamepata hifadhi katika Shule ya Upili ya Kituro, iliyo katika Baringo ya Kati.

“Ni jambo la kusikitisha kuwa tumewapoteza watu wawili katika ajali hiyo. Kumi wamehamishiwa katika MTRH ili kupata matibabu maalum, lakini wako katika hali nzuri. Wengine 51 watabaki leo katika hospitali ya Kabarnet ili hali zao kufuatiliwa,” akasema Dkt Kipsang.