Habari Mseto

WIZI WA KISHENZI: Mwanamume anaswa akiiba gurudumu ofisi za DCI

February 6th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MAAFISA wa polisi katika Idara ya Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) Jumanne walimkamata mwanaume ambaye alipatikana akiiba gurudumu katika eneo panapoegeshwa magari, katika makao makuu ya DCI, Nairobi.

Ofisi ya DCI ilisema kuwa Bw Wilson Kithome Muinde, mwanamume wa umri wa miaka 35 alipatikana akiiba gurudumu la ziada kutoka kwa gari nje ya makao yake.

Mshukiwa alikamatwa mara moja na kufikishwa kortini Jumatano, ambapo alifunguliwa mashtaka.

“Bw Wilson Kithome Muinde wa miaka 35 alikamatwa Jumanne na kufikishwa kortini Jumatano kwa kujaribu kuiba gurudumu la ziada kutoka kwa gari lililokuwa limeegeshwa katika makao makuu ya DCI,” idara hiyo ikasema kupitia akaunti yake ya Twitter.