Habari Mseto

Wizi wa mifugo unavyochochea uhaba wa walimu Pokot Magharibi

June 17th, 2024 1 min read

Na OSCAR KAKAI

KAUNTI ya Pokot Magharibi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, hali inayochangia shule za eneo hilo kuandikisha matokeo mabaya katika mitihani ya kitaifa.

Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) tawi la kaunti hiyo sasa kinaitaka Tume ya Huduma za Walimu Nchini (TSC) kuajiri walimu zaidi katika eneo hilo na maeneo mengine ya wafugaji.

Miongoni mwa sababu zinazochangia uhaba wa walimu katika kaunti ya Pokot Magharibii ni malipo duni na mazingira mabaya ya kufanyia kazi.

Hali hii huchangia idadi kubwa ya walimu kugura taaluma hiyo na kujiunga na sekta zingine zinazolipa mishahara bora au kuamua kujiunga na siasa.

Sababu nyingine inayochangia uhaba wa walimu ni utovu wa usalama kwani walimu wasio wa asili ya Pokot Magharibi huhofia kushambuliwa na kuawa na majangili.

Isitoshe, baadhi ya walimu wamestaafu au kufa kutokana na sababu za kimaumbile na nafasi zao hazijajazwa.

Hali hii ilisababisha baadhi ya walimu wakuu kusitisha usomeshwaji wa baadhi ya masomo.

Katika Shule ya Msingi na Sekondari Msingi (JSS) ya Naruoruo katika Pokot Kaskazini yenye wanafunzi 484 ina walimu watano pekee.

Mwalimu Mkuu Evan Kuya ambaye pia ni mwalimu wa JSS anasema shughuli za kuwafundisha wanafunzi zimetatizwa na hali hiyo.

“Hii ni changamoto kubwa na inapasa kushughulikiwa,” anasema.

Uhaba wa walimu walioajiriwa na serikali katika kaunti ya Pokot Magharibi umewalazimisha walimu kutoa fedha zaidi za kuajiri walimu wa vibarua.

“Tumelazimika kuuza mali yetu kuhakikisha kuwa walimu walioajiriwa na bodi za usimamizi wa shule kulipwa mishahara kwa wakati. Tunategemea walimu walioajiriwa na bodi za usimamizi ili kusaidia watoto wetu washindane na wengine kitaifa,” anasema Bw John Lokuk, mzazi kutoka Kacheliba.

Kaunti ya Pokot Magharibi ni mojawapo wa maeneo yanayoshuhudia utovu wa usalama Bonde la Ufa, wizi wa mifugo ukikithiri.

Licha ya serikali kutuma vyombo vya usalama kukabiliana na kero hiyo, baadhi ya shule zimefungwa kwa sababu ya visa vya mashambulizi.