Wizi wa mifugo wazidi kijijini Ngoingwa

Wizi wa mifugo wazidi kijijini Ngoingwa

Na LAWRENCE ONGARO

WIZI wa mifugo umezidi katika kijiji cha Ngoingwa mjini Thika, huku wakazi wa huko wakitaka serikali kuingilia kati.

Mnamo Jumatano usiku, ng’ombe wanne wa Bi Mary Njeri ambaye ni wa kijiji hicho, waliibwa ambapo zizi liliachwa wazi.

Alipata mifugo yake imeibwa zizini majira ya asubuhi.

“Niliamka asubuhi ambapo mfanyakazi wangu aliniarifu kuwa ng’ombe wanne walikuwa wameibwa kutoka zizini. Mmoja kati yao alikuwa na mimba ya miezi saba,” alisema Bi Njeri.

Alisema wezi hao huja usiku wa manane hasa mvua ikinyesha.

Alieleza kuwa hali hiyo imefanya wafugaji wengi kuwa na wasiwasi huku wakihofia mifugo yao itaisha serikali isipoimarisha usalama eneo hilo.

“Sisi tunataka serikali iingilie kati ili kunasa wezi hao ambao wameweka watu katika hali ya kiwewe,” alisema Bi Njeri.

Mkazi mwingine Bw Joseph Kimani ambaye hufuga nguruwe anasema wanne waliibwa ambapo hadi sasa hajawapata.

Alisema wezi hao huweka mikate pombe na kuwalisha nguruwe hao.

“Nguruwe hao hulewa chakari na baadaye hubebwa kwa pick-up na kutoweka. Tumeachwa katika hali ya wasiwasi,” alisema Bw Kimani.

Alisema hali ya usalama katika kijiji hicho pia haiko sawa na kwa hivyo ni vyema serikali iingilie kati.

“Baadhi ya mifugo ambao huibwa katika eneo hilo ni ng’ombe, nguruwe, kuku na mbuzi. Hata wakazi wengine wanaweka mifugo yao ndani ya nyumba,” alisema Bw Kimani.

Naye David Maina alisema hata wakazi wa huko wanaogopa kutoka usiku kwa sababu wezi hao huwa wamejihami kwa silaha hatari.

Alipendekeza walinda usalama wawe wakipiga doria kwa muda wa saa 24 ili kukabiliana na hali hiyo.

Alisema wangetaka machifu waandae vikao vya baraza kila mara ili wajadili kwa uwazi shida za eneo hilo.

You can share this post!

Wanasoka saba waliokosea kuondoka Barcelona wakiwemo Neymar...

DOMO KAYA: Ama kweli yote ni vanity!