Habari za Kaunti

Wizi wa pikipiki Taita Taveta wazua hofu

May 3rd, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

WAHUDUMU wa bodaboda katika Kaunti ya Taita Taveta wamelalamikia kurejea kwa visa vya wizi wa pikipiki katika eneo hilo.

Haya yanajiri kufuatia mauaji ya waendeshaji wawili wa bodaboda viungani mwa mji wa Voi huku pikipiki zao zikiibiwa.

Kulingana na takwimu za Chama cha Wahodumu wa Bodaboda Taita Taveta, pikipiki tano zimeibwa tangu mwaka 2024 uanze.

Wezi mara nyingi hulenga zile mpya.

Viongozi wa chama hicho walisema kuwa huenda visa hivyo vinatekelezwa na wahalifu wanaungana na waendeshaji wenzao.

Mnamo Aprili 2024, mwathiriwa wa kwanza, aliyekuwa na umri wa miaka 48, alipatikana akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa katika eneo la Ikanga huku pikipiki yake mpya ikikosekana.

Jumatano wiki hii, mhudumu mwingine alikutana na mauti na pikipiki yake pia ikaibiwa, visa vinavyotia wasiwasi waendeshaji wa bodaboda.

Wahudumu wanaoponea mikononi mwa majambazi hao huachwa na majeraha mabaya na hutupwa vichakani, hasa kwenye makorongo yaliyoko ndani ya shamba la Makonge la Voi.

Maafisa wakibeba mwili wa mhudumu wa bodaboda aliyeuawa na wezi mjini Voi. PICHA | LUCY MKANYIKA

Matukio haya yameibua maswali kuhusu hatua zilizowekwa na vikosi vya kulinda usalama ili kulinda wahudumu hao ambao mara nyingi huwa hatarini kutokana na asili ya kazi yao haswa usiku.

Ripoti zinaashiria kuwa pikipiki zilizoibiwa zinasafirishwa kimagendo hidi nchi jirani ya Tanzania kupitia mpaka wa Taveta/Holili.

Katibu Mkuu wa chama hicho cha bodaboda Bw Paul Chege, alisema genge linalowalenga waendeshaji pikipiki haswa zile mpya, limewatia hofu.

Alitoa wito kwa asasi za usalama kuchukua hatua za haraka ili kukomesha uhalifu huo.

“Wenzetu wanauawa, na inaonekana kama hakuna kinachofanyika,” alisema Bw Chege.

Alisema chama hicho na mashirika ya usalama katika eneo hilo wamepanga mkutano mnamo Jumamosi kujadili njia ya kukomesha uhalifu huo.

“Polisi wanahitaji kuimarisha usalama na kuboresha juhudi za ushirikiano kati yetu na wao ili tuweza kukabiliana na tishio hili la uhalifu. Wanatulaumu ilhali wanaendelea kutukamata kiholela ndio maana hatuwezi kufanya kazi pamoja,” alisema.

Akithibitisha matukio hayo, mkuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Voi Bw Ibrahim Dafalla alisema kuwa uchunguzi unaendelea.

Bw Dafalla alitoa wito kwa wahudumu hao kufanya kazi kwa karibu na idara ya usalama.

Bw Dafalla aliwasihi wahudumu hao kuwa waangalifu haswa wakati wa usiku na kuwahimiza kuripoti watu wowote wanaoshukiwa kwa polisi.

“Usalama unaanza na wao. Ni wao ndio watasaidia maafisa wa usalama kupambana na uhalifu. Hatuko kila mahali kwa hivyo nawasihi wawe mstari wa mbele katika kutoa taarifa muhimu kwetu,” alisema.

Baadhi ya wahudumu wa bodaboda wakiwa mjini Voi. PICHA | LUCY MKANYIKA

Mwenyekiti wa chama hicho Brian Tole alitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua kali zaidi, ikiwa ni pamoja na ushirikiano kati ya waendeshaji hao na vyombo vya usalama.

“Sisi pia tunawaomba wanachama wetu kuwa waangalifu wawapo kazini. Ikiwa una shaka na abiria anayetaka huduma, basi si lazima umbebe. Wanaweza pia kusindikizana,” alisema Bw Tole.