Habari Mseto

Wizi wapungua KCSE 2019

December 18th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

IDADI ya watahiniwa waliohusika kwenye udanganyifu wa mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu imepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2018.

Kulingana na Waziri wa Elimu Prof George Magoga, watahiniwa 1,309 ndio walioshiriki udanganyifu na hivyo watakosa matokeo yao.

Idadi hii ni ya chini kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka jana ambapo watahiniwa 4,519 walihusika katika kudanganya.

Prof Magoha alisema wanafunzi hao walipatikana na hatia ya kutumia mbinu mbalimbali kushiriki udanganyifu. Baadhi walitumia simu za mkononi, wengine wakibadilishana karatasi kwenye vyumba vya mtihani na wengine kufanya mtihani kwa niaba ya wenzao.

Prof Magoha alisema kuendelea kupungua kwa idadi hiyo kila mwaka kunatokana na mabadiliko makubwa yaliyotekelezwa kuanzia mwaka wa 2016 kwenye mchakato wa kutayarisha, kufanya na kusahihishwa kwa mitihani.

Katika kile kinachoonyesha watahiniwa wanaendelea kukumbatia matumizi ya simu kuiba mtihani, simu 47 zilinaswa mwaka huu ikilinganishwa na simu 20 mwaka wa 2018.

Kwa upande mwingine, wanafunzi walioingia na vifaa vya kufanikisha wizi wa mtihani walipungua kutoka 142 hadi 101 huku idadi ya waliozua mtafaruku kwenye vyumba vya mtihani ikisalia mtahiniwa moja pekee kama mwaka jana.

Profesa Magoha aliwarai wazazi ambao wanao ni watahiniwa kwenye mitihani ya kitaifa kuwaelekeza na kuwakanya dhidi ya kushiriki udanganyifu.