Habari

Waliopatikana na hatia ya kuua wanafunzi 145 kuhukumiwa Julai 3

June 19th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WANAUME watatu waliopatikana na hatia ya kuwaua wanafunzi 145 wa Chuo Kikuu cha Garissa na maafisa watano wa usalama miaka minne iliyopita watajua hatima yao Julai 3, 2019 watakapohukumiwa kwa hatia ya kufanya njama za kutekeleza ugaidi na kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Huku Rashid Mberesero, Hassan Edin Hassan na Muhamed Abdi Abikar wakirudishwa Gereza Kuu la Kamiti ambako wamekuwa tangu Aprili 2015, mshukiwa Sahal Diriye Hussein aliachiliwa huru.

Jumla ya washukiwa watano walikamatwa na kushtakiwa baada ya shambulizi hilo.Wawili kati yao Mabw Diriye na Osman Abdi Dagane wamekuwa na bahati ya mtende kwani waliachiliwa baada ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi kuamua “hawana hatia baada ya kuchambua ushahidi wote.”

Dagane aliyekuwa mlinzi chuoni humo alikamatwa kwa madai “ alimkuta akipiga picha za wanafunzi waliokufa na kurudikwa pamoja.”

Sahal Diriye Hussein aliyeachiliwa huru. Picha/ Richard Munguti

Diriye aliyefika kortini na Quran na Taspin alishinda siku nzima akisali. Aliamriwa atoke aende kwa “vile hakuna ushahidi wa kumlinganisha na mauaji hayo ya halaiki ya wanafunzi ambao shauku yao ya kisomo ilikatizwa na magaidi wanne ambao hawakuwakosea.”

Akitoa uamuzi dhidi ya Rashid Mberesero, Hassan Aden Hassan na. Muhamed Abdi Abikar, Bw Andayi alisema , “Nyinyi ni magaidi wa Al Shabaab. Mliwasiliana nao kwa siku kabla na wakati wa shambulizi hilo la kigaidi. Mlisababisha mauaji ya wanafunzi wasio na hatia.”

“Bila tashwishi yoyote mauaji hayo yalitekelezwa na magaidi wa Al Shabaab. Waliwaambia wanafunzi walikuwa wanatekeleza mauaji hayo kuilazimisha Serikali kuyaondoa majeshi yake nchini Somalia,” Andayi.

Rashid Mberesero aliyefumaniwa mvunguni mwa kitanda akiwa amevaa Kaptula siku ya shambulizi. Picha/ Richard Munguti

“Upande wa mashtaka ulioongozwa na wakili wa Serikali Duncan Ondimu umethibitisha kabisa nyinyi watatu mlikuwa mna wasiliana na magaidi hao waliokuwa wanatumia nambari ya simu 0725933614.”

Akaendelea kusema Andayi, “Kampuni ya Safaricom haikuwa na sababu ya kuunda njama na vitengo vya usalama kubuni nambari hii ya simu ya rununu iliyokuwa na magaidi wanne waliouawa kuwasiliana na Aden na Abdi.”

Aden alikamatwa akitoa Garissa Aprili 2, 2015 siku ya shambulizi akiwa ameabiri Bas la Kampuni ya Tawal akiwa na Abdi wakielekea Mandera.

Mberesero alikutwa na Polisi akijificha mfunguni mwa kitanda akiwa amevalia kaputula.

Hakimu mkuu Francis Andayi aliyewapata na hatia. Picha/ Richard Munguti

Hakuweza kueleza alichokuwa akifanya shuleni na hakuwa na kitambulisho.

Korti ilisema alishiriki katika mauaji ya wanafunzi hao na maafisa wa usalama

“Ulikataa kutoka mvunguni mwa kitanda ulipoamriwa na maafisa wa usalama. Ulishiriki katika mauaji hayo kwa kuwapelekea magaidi hao katika mabweni kwa vile ulikuwa unaelewa ramani ya chuo hivho,” hakimu alimweleza Mberesero.

Alisema Mberesero alikuwa ameishi mjini Garissa na mara kwa alikuwa akitoa mafunzo katika msikiti ulioko hapo mjini na kuwa mnamo Aprili 2, 2015 aliacha mfuko wake msikitini na kuondoka alfajiri kuungana na magaidi kutekeleza mauaji hayo ya kinyama.”