Michezo

Wolves, Newcastle na Everton miongoni mwa vikosi vinavyowania huduma za beki Maitland-Niles wa Arsenal

August 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WOLVES na Newcastle United wameanika wazi maazimio ya kumsajili beki wa Arsenal, Ainsley Maitland-Niles, 22, anayetazamiwa kuondoka rasmi uwanjani Emirates kufikia mwisho wa Agosti, 2020.

Difenda huyo mzawa wa Uingereza aliwajibishwa na Arsenal katika jumla ya mechi 32 za mapambano yote ya msimu huu wa 2019-20 na alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kilichowapepeta Chelsea 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA iliyochezewa ugani Wembley, Uingereza mnamo Agosti 1, 2020.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal wanapania kujisuka upya, na tayari wamemtia Maitland-Niles mnadani kwa pamoja na wanasoka wengine wakiwemo Matteo Guendouzi, Torreira, Mohamed Elneny, Shkodran Mustafi, Sokratis Papastathopoulos, Henrikh Mkhitaryan na Sead Kolasinac.

Mbali na Wolves na Newcastle, kikosi kingine ambacho kimefichua azma ya kumsajili Maitland-Niles ni Everton ambao wako radhi kuweka mezani kima cha Sh2.8 bilioni kwa minajili ya sogora huyu.

Maitland-Niles aliingia katika sajili rasmi ya Arsenal akiwa na umri wa miaka sita na mkataba wake wa sasa na kikosi hicho unatazamiwa kutamatika rasmi mnamo 2023.