Wolves wang’ata Liverpool na kuendeleza masaibu ya kocha Jurgen Klopp katika EPL msimu huu

Wolves wang’ata Liverpool na kuendeleza masaibu ya kocha Jurgen Klopp katika EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

WOLVERHAMPTON Wanderers ya kocha Julen Lopetegui iliendeleza masaibu ya kocha Jurgen Klopp katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2022-23 kwa kupokeza Liverpool kichapo cha 3-0 ugani Molineux.

Liverpool walishuka dimbani wakipania kukwepa kichapo cha tatu mfululizo katika EPL ugenini kwa mara ya kwanza tangu 2012. Hata hivyo, walijipata chini katika dakika ya tano baada ya kombora la Hwang Hee-chan kumbabatiza beki Joel Matip na kujaa wavuni.

Dakika saba baadaye, chombo cha masogora wa Klopp kilivuja zaidi baada ya Craig Dawson aliyekuwa akichezea Wolves kwa mara ya kwanza kufanya mambo kuwa 2-0.

Kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Liverpool walikuwa wamelenga shabaha kwenye lango la wenyeji wao mara moja pekee.

Hata hivyo, walirejea ugani kwa matao ya juu katika kipindi cha pili na nusura wafunge mabao mawili ya haraka kupitia kwa Andy Robertson, Mohamed Salah na Darwin Nunez waliomwajibisha vilivyo kipa Jose Sa.

Licha ya presha hiyo, Wolves walipata mpira wa kushtukiza na kufunga bao la tatu kupitia kwa Ruben Neves aliyemegewa krosi safi na Adama Traore.

Huku ushindi wa Wolves ukiwaondoa katika hatari ya kuteremshwa ngazi na kuwapaisha hadi nafasi ya 15 kwa alama 20, Liverpool walisalia katika nafasi ya 10 jedwalini kwa pointi 29.

Sasa ni pengo la alama 21 ambalo linatamalaki kati ya Liverpool na viongozi wa jedwali Arsenal waliokung’utwa 1-0 na Everton uwanjani Goodison Park. Hofu zaidi kwa Liverpool ni kwamba hawajashinda mechi yoyote ya EPL mwaka huu wa 2023.

Wolves watamenyana na Southampton na Bournemouth katika michuano miwili ijayo ya EPL huku Liverpool wakialika Everton kabla ya kuwaendea Newcastle United ugani St James’ Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Lionel Messi abeba PSG dhidi ya Toulouse katika Ligi Kuu ya...

MIKIMBIO YA SIASA: Kujiuzulu Mwakwere kuumiza Wiper Pwani

T L