Wolves wang’ata Palace na kufuzu kwa raundi ya nne ya Kombe la FA

Wolves wang’ata Palace na kufuzu kwa raundi ya nne ya Kombe la FA

Na MASHIRIKA

WOLVES walitinga raundi ya nne ya Kombe la FA msimu huu baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Crystal Palace mnamo Januari 8, 2021 ugani Molineux.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Wolves lilipachikwa wavuni na kiungo mvamizi raia wa Uhispania, Adama Traore katika dakika ya 35.

Kocha Nuno Espirito Santo alitegemea idadi kubwa ya wanasoka wake wa kikosi cha kwanza katika mechi hiyo na wangalishinda kwa idadi kubwa zaidi ya mabao iwapo wachezaji wake wangetumia vyema fursa nyingi walizozipata.

Palace ambao walikifanyia kikosi chao kilichoshinda Sheffield United ligini mabadiliko tisa, hawakuelekeza kombora lolote langoni pa Wolves waliokuwa wenyeji wao.

Japo kocha Roy Hodgson aliwaleta ugani wanasoka Wilfried Zaha na Andros Townsend katika kipindi cha pili, uwepo wao haukutikisa uthabiti wa Wolves waliomiliki asilimia kubwa ya mpira na kuonekana kuwazidi maarifa wapinzani wao katika takriban kila upande.

Wolves waliingia ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kulazimishiwa sare ya 3-3 na Brighton katika mechi yao ya awali ligini.

Mbali na Traore aliyemhangaisha sana beki Patrick van Aanholt wa Palace, mwanasoka mwingine wa Wolves aliyejituma vilivyo katika mchuano huo ni fowadi Pedro Neto aliyeshirikiana vilivyo na viungo Leander Dendoncker na Fabio Silva.

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Tuzo za washindi wa Kombe la FA zapunguzwa kwa...

Liverpool wazamisha makinda wa Aston Villa na kusonga mbele...