Wolves wang’ata Southampton na kupaa kwenye jedwali la EPL

Wolves wang’ata Southampton na kupaa kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

PEDRO Neto alifunga bao lililowawezesha mbwa-mwitu Wolves kuwang’ata Southampton 2-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani St Mary’s.

Southampton ndio waliotangulia kufunga bao baada ya kuwekwa uongozini na mshambuliaji Danny Ings katika dakika ya 25 kabla ya Ruben Neves kusawazisha mambo katika dakika ya 53 kupitia mkwaju wa penalti.

Bao lililopachikwa wavuni na Ings lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Stuart Armstrong.

Penalti ambayo refa Graham Scott aliwapa Wolves waliokuwa wakichezea ugenini ilikuwa zao la tukio la  Ryan Bertrand kumchezea visivyo beki Nelson Semedo aliyesajiliwa na Wolves mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 kutoka Barcelona.

Bao la Neto katika dakika ya 66 lilitokana na ujanja uliomwezesha kumpiku kirahisi Jannik Vestergaard kabla ya kumtoka Jan Bednarek na kumwacha hoi kipa Alex McCarthy.

Japo Southampton walipania kusawazisha, wageni wao walisalia imara huku kipa Rui Patricio akifanya kazi ya ziada kudhibiti makombora ya James Ward-Prowse na Che Adams.

Ushindi wa Wolves uliwapaisha jedwalini hadi nafasi ya 12 kwa alama 30, moja zaidi kuliko Southampton an Crystal Palace.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 75

UIGIZAJI: Harriet Kwamboka Charles aamini anacho kipaji cha...