Michezo

Word Warriors washuka baada ya kipigo

July 22nd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha taifa cha mchezo wa Scrabble almaarufu ‘The Word Warriors’ kiliteremka hadi nafasi ya tatu kwenye Kundi C katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea mitandaoni.

Kenya iliyowapiga Singapore katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi C, ilipokea kichapo cha 18-7 kutoka kwa Canada katika mechi ya pili.

Ushindi mwingine dhidi ya Canada ungaliwapa Kenya tiketi ya kushiriki robo-fainali. Hata hivyo, ni Canada kwa sasa ndio wanaoselelea kileleni mwa Kundi C mbele ya Singapore waliowatandika Ghana 21-4 katika mechi yao ya pili kundini.

Licha ya vijana wake kuzidiwa maarifa na Canada, Bernard Amuke ambaye ni Mwenyekiti wa Scrabble Kenya, ni mwingi wa matumaini kwamba Kenya ingali na nafasi ya kutinga hatua ya robo-fainali iwapo itawaangusha Ghana katika mchuano wao wa mwisho wa Kundi C wikendi hii.

“Mechi dhidi ya Canada ilikuwa ngumu. Hata hivyo, tungali na matumaini ya kufuzu kwa kuwa tuna wingi wa matarajio ya kuwapepeta Ghana katika mechi ya mwisho. Ingawa hivyo, kufuzu kwetu kutategemea pia na iwapo Canada itawazamisha Singapore katika mchuano wa kufunga mapambano ya makundi,” akasema Amuke.

Wakicheza kwa mfumo wa mzunguko ambapo mshiriki hukutana na washindani wote wengine (round-robin format), wachezaji wa Kenya walipoteza raundi zao zote kwa seti za (1-4, 1-4, 2-3, 1-4 na 2-3).

Katika mechi za raundi ya ufunguzi, Canada iliwazaba Ghana 13-12 huku Kenya ikiwapepeta Singapore 11-8.