Makala

Wosia wa Moi sasa kusomwa kortini ijulikane nani alipata nini kukomesha mzozo

Na RICHARD MUNGUTI August 15th, 2024 2 min read

WARITHI wote wa mali ya Hayati Rais Daniel arap Moi Jumatano waliagizwa wafike kortini Oktoba 7, 2024 wakati wa kuthibitishwa kwa Wosia wake kuhusu ugavi wa mali yake zaidi ya Sh300 milioni.

Jaji Hilary Chemitei alitoa agizo hilo alipoahirisha kusikizwa kwa kesi iliyoshtakiwa na Milkah Faith Nyambura mmoja wa wajane wa mwanawe Jonathan Kipkemoi Toroitich, aliyeaga Aprili 2019.

Jaji Chemitei aliwaelekeza mawakili Julius Kemboy (wa familia ya hayati Moi) na Duncan Okatchi anayewakilisha Milkah wafike kortini Oktoba 7, 2024 Wosia wa Moi uthibitishwe.

Bw Kemboy alieleza mahakama kwamba Moi ameeleza kinaga ubaga jinsi angelipenda mali yake igawanywe atakapoaga.

Mabw Kemboy na Okatchi walieleza mahakama kwamba wanawe watano wa hayati Moi hawajazozana kuhusu ugavi wa mali yake na hivyo basi “kilichoko ni kuthibitisha Wosia huo ndipo msimamizi Zehrabhanu Jan Mohammed agawe mali yake.”

Mawakili hao walieleza mahakama kwamba wajukuu na wajane wa wana wa hayati Moi hawapasi kupewa urithi moja kwa moja kutoka kwa mali ya rais huyo wa pili wa Kenya.

Milkah ambaye ni mmoja wa wajane wa Jonathan, aliwasilisha kesi akiomba mahakama iamuru apewe Sh2.5m za kugharamia matibabu ya  mwanawe Gift Moi.

Wakiomba kesi hiyo iahirishwe Mabw Kemboy na Okatchi walisema wahusika wote katika kesi wanapasa kuthibitisha Wosia huo ndipo ugavi ufanywe.

Katika Wosia huo, Moi aliyeaga dunia Feburuari 4, 2020 aliwaorodhesha wanawe watano—Jonathan, Raymond, John Mark, Philip na Gideon kuwa warithi.

Mahakama ilielezwa mali ya hayati Moi imewekwa chini ya Wafadhili wa Wakfu wake.

Mali yake ni pamoja na shamba la ekari 931 ambapo Chuo Kikuu cha Kabarak kimejengwa.

Alisema wanawe watano warithi shamba hilo.

Moi alisema katika Wosia huo wanawe watano wakifa, wajukuu wake wanaume warithi shamba hilo.

Kuhusu bintize – Jennifer, Dorris Chepkorir na June Chebet (aliyefariki hivi majuzi) aliamuru wapewe Sh100 milioni kila mmoja.

Moi aliandika Wosia huo mnamo Novemba 15, 2005 na kuufanyia marekebisho Machi 30, 2010.

Kuna kesi nyingine pia ya urithi.

Jaji Chemitei aliwaambia mawakili Kemboy na Okatchi ameusoma Wosia huo na haujaeleza mambo mengi ila jinsi mali yake itakavyogawa.