Michezo

Xhaka aonyeshwa kadi nyekundu Burnley wakizidisha masaibu ya Arsenal katika EPL

December 14th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

GRANIT Xhaka alionyeshwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu katika mchuano ulioshuhudia Arsenal wakizomewa na kurushiwa cheche za matusi baada ya kupigwa 1-0 na Burnley katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Emirates, mnamo Jumapili.

Kushindwa kwa Arsenal kunamaanisha kwamba kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta sasa kimepoteza mechi nne mfululizo katika uwanja wa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu 1959.

Bao lililowavunia Burnley alama tatu muhimu dhidi ya Arsenal lilifumwa wavuni na Pierre-Emerick Aubameyang aliyejifunga katika dakika ya 73. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Burnley kushinda Arsenal tangu Septemba 1974.

Vijana wa kocha Sean Dyche waliteremkia Arsenal na kuvuna ushindi huo baada ya Xhaka kufurushwa uwanjani katika dakika ya 58 kwa kumkwida kiungo wa Burnley almaarufu Clarets, Ashley Westwood.

Japo awali Xhaka alionyeshwa kadi ya manjano, refa Graham Scott alibatilisha maamuzi hayo na kumchomolea raia huyo wa Uswisi kadi nyekundu baada ya kurejelea video ya tukio hilo kwenye mtambo wa teknolojia ya VAR.

Ingawa Arsenal walipata fursa nyingi za kuwafunga Burnley, bahati haikusimama nao huku kipa Nick Pope akipangua kirahisi makombora aliyoelekezewa na Alxandre Lacazette na Bukayo Saka.

Alama tatu zilizotiwa kibindoni na Burnley ziliwatoa kwenye mduara unaoshikiliwa na vikosi vilivyopo katika hatari ya kuteremshwa ngazi. Arsenal kwa upande wao walisalia katika nafasi ya 15 kwa alama 13 kutokana na mechi 12 za hadi kufikia sasa muhula huu.

Arteta ataadhimisha mwaka mmoja akiwa kocha wa Arsenal mnamo Disemba 26, 2020. Ingawa matarajio ya mashabiki yalikuwa makuu alipowaongoza waajiri wake kutwaa Kombe la FA mwishoni mwa msimu jana na kutwaa taji la Community Shield mwanzoni mwa msimu huu, matumaini hayo yanazidi kudidimia.

Japo wametinga hatua ya mwondoano kwenye Europa League, fomu ya Arsenal ligini ni ya kusikitisha zaidi nyumbani na ugenini ambapo wamepoteza jumla ya mechi saba kati ya 10 zilizopita.

Ni rekodi mbovu ambayo imechochea mashabiki kuuliza maswali zaidi kuhusu uwezo wa Arteta pamoja na mbinu zake za ukufunzi ambazo zinaelekea kuwaweka Arsenal katika hatari ya kushushwa ngazi msimu huu baada ya kutozaa matunda ligini.

Ubutu wa Arsenal mbele ya malango ya wapinzani wao sasa umewafanya kushuhudia ukame wa mabao kwa kipindi cha saa 12 na dakika 32 kwenye kampeni za EPL msimu huu.

Baada ya Mesut Ozil kutemwa kwenye kikosi cha kwanza, Arsenal wamesalia bila kiungo mpakuaji aliye na uwezo wa kutoa krosi za hakika na kuwaandalia washambuliaji wao nafasi nzuri za kufunga mabao.

Ilivyo, mfumo anaotumia Arteta kwa sasa unasaza Arsenal katika ulazima wa kutegemea zaidi maarifa ya chipukizi Saka na Willian ambao wamekuwa wakizidiwa nguvu na mabeki wa wapinzani pembezoni mwa uwanja.

“Tuliwapa Burnley alama za bure. Tulianza vyema mechi hiyo na tukaidhibiti vilivyo. Mambo yalianza kubadilika baada ya Xhaka kuonyeshwa kadi nyekundu. Wageni wetu walitulemea katika kila idara,” akasema Arteta.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Southampton uwanjani Emirates mnamo Disemba 16 huku Burnley wakiwaendea Aston Villa ugani Villa Park.