TAHARIRI: Ya Mwendwa yameisha, tuboreshe soka sasa

TAHARIRI: Ya Mwendwa yameisha, tuboreshe soka sasa

Na MHARIRI

HATIMAYE mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), Nick Mwendwa, alijuzulu wadhifa wake mnamo Jumanne usiku na kumwachia mamlaka naibu wake Doris Petra.

Mwendwa anakumbwa na kesi ya ufisadi kortini ambako ameshtakiwa kwa ubadhirifu wa Sh38 milioni za FKF, baada ya kukamatwa mara mbili na makachero kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) mara mbili Novemba.

Hata hivyo, hatua hiyo huenda isiwe na maana kwani FKF ilishavunjiliwa mbali na serikali.

Kwa kuwa Mwendwa ameondoka FKF, sasa ni wakati ambapo kamati ya muda iliyoundwa na Waziri Amina Mohamed, ihakikishe kuwa soka ya nchi inakwea ngazi na kufikia viwango vya juu kama nchi nyingine.

Kwanza, ni vyema kuwa kamati hiyo ishatoa ratiba mpya ya Ligi Kuu (KPL) huku mechi zikirejelewa wikendi hii katika nyuga mbalimbali, baada ya kusitishwa kwa majuma matatu yaliyopita kufuatia kuvunjwa kwa FKF.

Ili ligi hiyo iendeshwe vyema, serikali ihakikishe timu zote 18 zinapewa pesa kutoka Hazina ya Michezo, kwa sababu ligi kwa sasa haina mdhamini baada ya kujiondoa kwa kampuni ya kamari ya BetKing mwishoni mwa msimu jana.

Pesa hizo zitasaidia wachezaji na klabu kujikimu huku kamati ikiendelea kusaka mdhamini mpya wakati ambapo itakuwa usukani, kabla ya uchaguzi mwingine wa FKF kuandaliwa.

Pili, serikali kupitia kamati hiyo inafaa kuwalipa waamuzi na pia kuhakikisha kuna pesa za kutosha kuendesha Ligi yaKitaifa ya Supa (NSL), ile ya Wanawake na ligi nyingine za chini ambazo zipo chini ya FKF.

Tatu, katika kuhakikisha kuwa soka inasonga mbele baada ya miaka sita ya utawala chwara wa Mwendwa, kamati simamizi inafaa kusaka pia kampuni ya kupeperusha matangazo kuhusu mpira wetu jinsi ilivyokuwa enzi za KPL kupitia kampuni ya SuperSport.

Kando na hayo, kamati hii inafaa kusaka kocha mpya wa timu ya taifa Harambee Stars; awe amehitimu vizuri na mchapakazi.

Wakati wa utawala wa Mwendwa matokeo ya Stars yalidorora mno huku tukilemewa na hata timu dhaifu zaidi barani Afrika.

Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Kenya haikuwa na wapinzani wagumu kama miaka ya nyuma ila ilishindwa huku ikifunga Rwanda pekee na kupata matokeo yasiyoridhisha dhidi ya Mali na Uganda.

Na iwapo mwishowe uchaguzi mwingine wa FKF utaandaliwa baada ya miezi sita iwapo mahakama itadumisha uamuzi wa kuunda kamati ya mnamo Disemba 16, basi matawi ya FKF yahakikishe anayechaguliwa anasimamia vyema soka yetu.

Kuendesha mpira kwa kifua na kudhulumu baadhi ya timu jinsi alivyofanya Mwendwa dhidi ya Gor Mahia na AFC Leopards kusitokee tena bali uongozi huo uhakikishe unasaka talanta na kukuza wachezaji wachanga.

Kwa sasa, macho na juhudi zote zielekezwe katika kuboresha mpira wetu wala si uhasama kati ya serikali na Mwendwa.

You can share this post!

Mlipuko usiku waibua hofu kijijini Lamu

Idadi ya wanaotumia ARVs yapanda kwa asilimia 83 –...

T L