Habari MsetoSiasa

Yabainika gari la seneta lililodaiwa kuibwa lilitwaliwa na madalali

June 11th, 2018 1 min read

Na WANDERI KAMAU

GARI la aliyekuwa Seneta Maalum Paul Njoroge lilitwaliwa na madalali Ijumaa usiku, kinyume na madai kwamba lilikuwa limeibwa.

Mnamo Jumamosi, Bw Njoroge aliripoti kwa polisi kwamba gari hilo aina ya Toyota V8 lilikuwa limeibwa nyumbani kwake katika eneo la Kitengela.

Hata hivyo, ilibainika jana kwamba gari hilo lilitwaliwa na kampuni ya madali ya Acceptance Limited Kenya, baada ya Bw Njoroge kushindwa kulipa mkopo wa Sh3 milioni aliochukua kutoka kwa kampuni hiyo.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo Bw James Nyagah, Bw Njoroge alikuwa amekiuka taratibu za ulipaji wa mkopo huo, hata baada yao kuafikiana kuhusu muda ambao angechukua kumaliza kulipa.

Alisema Bw Njoroge alikuwa akifahamu kwamba gari hilo lingetwaliwa, kwani amekuwa akilificha kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa.

Mwaka uliopita, Bw Njoroge alizua kizaazaa baada ya kutisha kumpiga risasi aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Mafuta ya Vivo, Polycarp Igathe baada ya tofauti za usimamizi wa kituo chake cha mafuta mjini Naivasha kuzuka.