Habari Mseto

Yabainika upatanisho wa Sonko, Badi ulikwama

September 2nd, 2020 1 min read

Na COLLINS OMULO

KUNDI la kutatua mzozo kati ya Gavana Mike Sonko na Idara ya Huduma ya jiji la Nairobi (NMS), limeomba liongezewe siku 30 kushughulikia masuala yaliyozua uhasama kati ya pande hizo mbili.

Imebainika hatua hiyo imechukuliwa baada ya pande hizo mbili kushindwa kukubaliana kuhusu masuala yaliyoibua mizozo kati yao, na sasa Mwanasheri Mkuu atahitajika kuingilia kati.

Kundi hilo linaloongozwa na Wakili Mkuu wa serikali, Bw Ken Ogeto limekuwa likikutana tangu kati kati ya Agosti kutafuta muafaka.

Mazungumzo hayo yalitokana na agizo la mahakama iliyopatia pande zote siku 90 kuhalalisha mkataba wa kuhamisha majukumu kwa serikali ya kitaifa Gavana Sonko alipolalamikia utekelezaji wa mkataba huo.

Kufikia sasa, kundi hilo limekutana mara tatu katika ofisi za Mwanasheria Mkuu. Mahakama ilikuwa imepatia pande zote hadi Septemba 18, 2020.

Pande zote hazikuweza kukubaliana kuhusu masuala yaliyozua mzozo na Bw Ogeto akaomba serikali ya kaunti kupatia upande wake siku 30 zaidi kujadiliana.

“Tulifanya mkutano wa tatu Alhamisi wiki iliyopita na Mwanasheria Mkuu akaomba siku 30 kutatua mzozo huo ombi ambalo serikali ya kaunti ilikubali,” alisema mmoja wa wanaohusika na mazungumzo hayo.

NMS na serikali ya Sonko hawajakubaliana kuhusu mfumo wa kufadhili NMS, suala la nyumba ya gavana, kuhamishwa kwa wafanyakazi wa serikali ya kaunti hadi NMS na ulipaji wa madeni na kandarasi.

Msemaji wa Bw Sonko, Ben Mulwa alisisitiza kuwa masuala ya fedha hayakuhamishwa na akalaumu NMS kwa kutwaa baadhi ya majukumu kinyume na mkataba.