Habari Mseto

Yabainika viwanja viwili vya ndege havina hati

March 14th, 2018 2 min read

Na LUCY KILALO

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (KAA) imeagizwa kufafanua ni vipi haina hatimiliki za ardhi ya Kiwanja cha Ndege cha Manda, Kaunti ya Lamu na kile cha Kisumu.

“Itakuwaje ikiwa mtu atatokezea na kudai ardhi hii?” aliuliza mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uwekezaji wa Umma, Abdulswamad Shariff Nassir.

Wasimamizi wa mamlaka hiyo ambao walikuwa wamefika mbele ya kamati hiyo kujibu maswali ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Umma, hawakuweza kufafanua kuhusu ziliko stakabadhi hiyo.

Bw Nassir alitaka pia kujua kwa nini baadhi ya hati miliki za ardhi ya viwanja vya Wilson, Eldoret ziko na mawakili, na ile ya Ukunda kuripotiwa na wasimamizi kuwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

“Tutajuwaje kuwa hati miliki hazijatumiwa kuchukulia mikopo?” aliuliza mwenyekiti.

“Ikiwa zilipotea, ziliwahi kuripotiwa kupotea? Hii ni kwa sababu tunaona mashirika ya serikali hata yakiweka matangazo magazetini ya vitabu vya risiti vilivyopotea,” alisema Bw Nassir.

 

Hofu

Mbunge wa Kiminini, Bw Chris Wamalwa, pia alielezea hofu yake kuwa isiwe kuwa ardhi hiyo imetumika kama rehani kuchukua mikopo mikubwa ambayo hatimaye, inafanya nchi zilizotoa mikopo kuichukua.

Afisa Mkuu mtendaji wa mamlaka hiyo, Jonny Andersen hata hivyo, alikana suala la wao kutumia ardhi hiyo kwa mikopo.

Hata hivyo, Bw Andersen aliahidi kuhakikisha kuwa wanawasilisha majibu yanayohitajika kuhusiana na hati miliki hizo.

Wakili wa kampuni, Bi Katherine Kisila, alikuwa na wakati mgumu kuelezea kuhusu hati miliki hizo, hata baada ya kuelezea kamati kuwa yeye ndiye anayestahili kuzihifadhi.

Kamati hiyo iliagiza mamlaka hiyo ihakikishe kuwa inawasiliana na Tume ya Kitaifa ya Ardhi, kubainisha ukweli kuhusu hati miliki hizo, pamoja na mawakili husika kuelezea sababu za kuwa wenye kuhifadhi hati miliki hizo.

 

Kandarasi za nyua

Mamlaka hiyo pia inakabiliwa na maswali mengine ya kuelezea sababu za kandarasi mbili ya kuweka ua katika mtaa wa Embakasi, na uwanja wa ndege ya

Ukunda za Sh24.5 milioni na Sh8.9 milioni zilifutiliwa mbali na kulazimu wakandarasi kulipwa kwa kukatiza mkataba.

Wanakamati hiyo walihofia kuwa miradi hiyo ilikuwa njama ya kufuja pesa za umma.

Mamlaka hiyo pia ilihitajika tena kuelezea vipi kampuni ya kibinafsi ya Transglobal iliongezewa muda wa kukodisha ardhi yake kutoka miaka 20 hadi 40 na ni vipi kampuni ilichukua mkopo wa zaidi ya Sh500 milioni.

Kamati hiyo ilielezea kuwa itamuita Waziri wa Fedha pamoja na Benki ya Standard Chartered kufafanua zaidi masuala hayo.

“Mkopo ulitolewa kwa madhumuni yapi, na ni nani aliyeidhinisha muda wa kukodi kutoka moaka 20 hadi 40?” aliuliza Bw Nassir.

Mkaguzi Mkuu Edward Ouko katika ripoti yake amekosoa masuala ya kifedha katika mamlaka hiyo ambayo huenda yakafanya mlipaji kodi kupoteza mabilioni ya pesa.