Habari

Yafichuka gaidi alikodi chumba Nairobi karibu na Kituo cha Polisi cha Central

February 19th, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MMOJA wa washukiwa wa ugaidi aliyekamatwa na shehena ya silaha alikodisha chumba cha malazi katika hoteli moja karibu na Kituo Cha Polisi cha Central jijini Nairobi, siku kumi kabla ya kukamatwa katika eneo la Merti, Kaunti ya Isiolo.

Abdimajit Adan, 24, wa kitambulisho cha kitaifa nambari: 32480689, alikamatwa pamoja na Mohammed Nane Alhamisi, wiki iliyopita akiwa na bunduki tano aina ya AK 47 na mifuko 36 ya risasi.

Kulingana na ripoti ya polisi, wawili hao walikamatwa baada ya kufyatuliana risasi na maafisa wa usalama. Nane alipigwa risasi na kufariki papo hapo.

Polisi walifahamishwa kuhusu gari nambari KBM 200D lililokuwa limefichwa msituni na raia wema.

Makabiliano dhidi ya washukiwa hao yaliongozwa na Naibu Kamanda wa Polisi wa Merti Maiyo Julius na Kamanda wa Polisi Gifinalis Barasa.

Jumatatu, meneja wa hoteli hiyo aliambia Taifa Leo kuwa mshukiwa huyo aliwasili hotelini hapo na kukodisha chumba mnamo Februari 9. Aliishi hotelini hapo kwa siku tisa na kisha kuondoka Alhamisi Februari 15.

“Alhamisi jioni maafisa wa polisi wa Kitengo cha Kukabiliana na Ugaidi (ATPU) walikuja hotelini hapa na kuniambia kuwa mmoja wa wateja wangu alikamatwa,” akasema.

Polisi walipoingia ndani ya chumba hicho walipata nguo za mshukiwa na tiketi ya ndege ya kutoka Elwak, Kaunti ya Turkana hadi uwanja wa Wilson, jijini Nairobi.