Habari MsetoSiasa

Yafichuka Ikulu inalazimisha Mlima Kenya kuunga mkono BBI

June 18th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

KATIBU wa Baraza la Mawaziri, Kennedy Kihara amefichua kuwa ni msimamo wa Rais Uhuru Kenyatta kuwa mrengo wa kisiasa wa Tangatanga kutupilia mbali siasa za 2022, na badala yake uzindue harakati za kuhimiza wenyeji waunge mkono ajenda ya BBI.

Bw Kihara amesema kuwa rais amesisitizia wandani wake kuwa hapo ndani ya BBI ndipo kuna afueni kuu ya baadaye kiuchumi na kisiasa kwa wenyeji wa Mlima Kenya.

Bw Kihara alisema kuwa “kamwe hakuna vile Rais Uhuru atasikizana na mrengo huo wa Tangatanga ikiwa utazidi kuendeleza siasa za urithi wa urais 2022 na ambapo huunga mkono Naibu wa Rais Dkt William Ruto katika urithi huo.

“Kwa mujibu wa Kihara, wanatangatanga wanaendeleza siasa za kujitafutia umaarufu badala ya wanza waungane na viongozi wengine na wenyeji Mlima Kenya kusaka mstakabali wa kuhakikishia eneo hilo usalama wa rasilimali na ugavi wa nyadhifa katika serikali zijazo.”

Alishikilia kuwa kwa sasa Rais Uhuru analenga kuacha Mlima Kenya katika safu thabiti ya kisiasa na kiuchumi “na kamwe hatakubali watu wake waingizwe na wanasiasa wasiojali upana wa utafsiri wa haki kwa wenyeji Mlima Kenya kwa mtego wa kisiasa usio na manufaa ya kirasilimali na nyadhifa serikalini.”

Bw Kihara alisema kuwa Rais ako na maono mema kuhusu wenyeji wa Mlima Kenya la mno likiwa ni “kuwahakikishia kuwa katika serikali zijazo, idadi ya watu na ubabe wa kura umetambulika kama kigezo kikuu cha ugavi wa rasilimali na nyadhifa katika serikali zijazo.”

Alisema kuwa ikiwa BBI itapitishwa na iwe sheria, “basi eneo la Mlima Kenya na idadi yake kubwa ya watu na kura zisizopungua Milioni Sita litanufaika na halitawahi kujali ni nani atakuwa Rais kwa kuwa huduma bora na za haki kwao zitakuwa zimelindwa kikatiba.”

Bw Kihara alisema kuwa kwa sasa Rais hatavumilia na wala hatakuwa na wakati wa kupoteza na wakereketwa wa siasa za 2022 eneo hilo la Mlima Kenya “huku wenyeji wakiwa katika kila kona ya kumfikia rais wanalalama kuhusu maendeleo duni na ukosefu wa umoja wa kisiasa.”

Alisema kuwa kwa sasa rais anasukuma kwa undi na uvumba eneo hilo lipate haki yake ya kimaendeleo sawa na maeneo mengine ya nchi.

“Rais halali na kila kuchao anafuatilia jinsi maendeleo yanasambazwa katika kila pembe ya nchi, Mlima Kenya ikiwemo. Ukiangalia bajeti ya 2020/21 ambayo imeandaliwa itakupa ushahidi wa hali hii kwa kuwa eneo hili limetengewa pesa za barabara, maji, stima…huku kukiwa na wanasiasa ambao hawataki kufuatilia utekelezaji huo na kila wakati wanasumbua rais na siasa za 2022,” akasema.

Bw Kihara ambaye ni mzawa wa Kaunti ya Murang’a alitoa mfano wa baadhi ya viongozi wa Tangatanga ambao husikika wakiteta kuwa “mawaziri na makatibu wa serikali ya Rais Uhuru wanatumia miradi ya kimaendeleo nyanjani katika maeneo yao ya kuzaliwa kujijenga kisiasa.”

Bw Kihara alisema kuwa hiyo ni kasumba ya kipumbavu “ambayo haiwezi ikamfaa mwananchi kwa lolote kwa kuwa maendeleo yakitekelezwa huwa ni kwa manufaa ya wote bali sio kwa mtu binafsi.”

Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria mara kwa mara husikika akiteta kuwa Katibu wa Maji, Peter Wairagu hutumia miradi ya maji kujipigia debe ili awanie ugavana 2022 kwa kuwa ni mzawa wa eneo hilo.

Aidha, Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia husikika akiteta kuwa Waziri wa Maji Bi Sicily Kariuki huonekana nyanjani akipeana miche ya maparachichi ili kujiweka pema kuwania ugavana eneo hilo 2022, sawa na katibu wa usalama wa Ndani, Karanja Kibicho ambaye amekuwa akilaumiwa na serikali ya Kaunti ya Kirinyaga kwa kuzindua miradi eneo hilo akisingiziwa hali ambayo huteteshwa huwa na siasa fiche za 2022.