Habari

Yafichuka jinsi watumishi wa umma wanavyofyonza nchi

November 23rd, 2019 2 min read

Na PAUL WAFULA

WATUMISHI wa umma wanaendelea kufyonza nchi kupitia marupurupu wanayodai kila mwezi kwa kazi waliyoajiriwa kutekeleza yanayowafanya wapate mishahara minono bila kuchoka.

Hii inafanya mfanyakazi wa serikali ya Kenya kupata mshahara wa wastani wa Sh78,000 kila mwezi na kuwa wanaopata mshahara bora zaidi katika nchi za eneo hili.

Kulingana na Tume ya Mishahara na Marupurupu nchini (SRC), Kenya hutumia Sh795 bilioni kila mwaka kulipa wafanyakazi wa umma wapatao 842,900 mishahara yao.

Hii inamaanisha kuwa, kwa wastani, wafanyakazi wote wa umma wangelipwa mishahara sawa, kila mmoja angepata Sh930,000 kwa mwaka.

Mwenyekiti wa SRC, Lyn Mengich, anasema kwamba japo Wakenya hudhani mishahara ya watumishi wa umma ni ya chini, kuna wanapata mishahara minono kila mwezi kwa sababu ya marupurupu.

“Kuna wakati asilimia 75 ya mishahara huwa ni marupurupu. Tunapaswa kukoma kuangalia mshahara wao wa kawaida pekee,” alisema Bi Mengich.

Ingawa watumishi wa umma huwa wanadai marupurupu kwa kazi waliyoajiriwa kufanya, hakuna anayewachukulia hatua.

Utafiti wa SRC ulifichua kuwa kuna aina 149 za marupurupu wanayolipwa watumishi wa umma ambayo wanatumia ujanja kufyonza walipa ushuru.

Kwa mfano, mfanyakazi mmoja ambaye mshahara wake ni Sh32,367, alipata Sh158,487 baada ya kudai marupurupu. Hii inamaanisha alipata Sh126,120 zaidi ya mshahara wake au asilimia 80 ya mshahara wa kawaida wa kila mwezi.

Utafiti wa SRC ulibainisha kuwa kati ya asilimia 65 na 85 ya mishahara ya kila mwezi ya watumishi wa umma wa viwango vyote huwa ni marupurupu.

Kwa wale watumishi wajanja, asilimia 95 ya mshahara wao wa kila mwezi huwa ni marupurupu.

SRC inayopanga kongamano la mishahara Jumanne inasema kuwa hakuna mipango ya kupunguza watumishi wa umma ikizingatiwa kuwa sekta za afya na elimu zinahitaji wafanyakazi zaidi.

Ikizingatiwa kuwa mwaka jana Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ilikusanya Sh1.58 trilioni, inamaanisha kuwa nusu ya mapato ya serikali hutumiwa kulipa mishahara pekee.

Na kwa kila Sh100 Wakenya wanazolipa ushuru, Sh50 hutumiwa kulipa mishahara na kuacha Sh50 kutumiwa kuendesha serikali kuu na za kaunti. Hii inafanya serikali kukopa pesa za kufadhili miradi ya maendeleo.

Deni la Kenya kwa wakati huu ni Sh6 trilioni na linatazamiwa kuongezeka baada ya bunge kuruhusu serikali kukopa hadi Sh9 trilioni.

Kulingana SRC, gharama ya juu ya mishahara hunyima serikali pesa za maendeleo na kuathiri ukuaji wa uchumi.