Habari MsetoSiasa

Yafichuka magavana hukodisha ofisi na kufanyia kazi Nairobi

April 7th, 2019 1 min read

JUSTUS WANGA Na KENNEDY KIMANTHI

MIAKA sita baada ya ugatuzi kuanza kazi nchini, magavana wengi bado wanaendesha kaunti zao wakiwa Jijini Nairobi, hali ambayo inamlimbikizia mzigo zaidi mlipa ushuru.

Hali hii inadunisha lengo la uongozi wa ugatuzi, ambalo lilikuwa kuondoa rasilimali Nairobi na kuzipeleka katika maeneo tofauti ya nchi.

Visa kadhaa vimeripotiwa ambapo magavana wanafanyia kazi Nairobi katika ofisi za kukodi, hotelini ama manyumbani kwao jiji kuu.

Wiki tatu zilizopita, katibu wa kaunti moja alilazimika kutumia ndege kufika Nairobi kumfikishia mkubwa wake nakala za malipo azitie sahihi, ilipobainika kuwa gavana huyo alikuwa akitaka kusafiri nje ya nchi na alikuwa amekosekana kwenye kaunti siku kadhaa.

Katika kaunti nyingine ya Nyanza mwezi uliopita, mawaziri waliitwa kwa mkutano wa baraza Nairobi, katika hali ambayo sasa inabainika kuwa ni mazoea.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa takriban magavana 30 wanafanyia kazi Nairobi, hali ambayo inazidisha gharama za matumizi ya kaunti, sakata ambayo huenda Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za umma Edward Ouko akafichua.

Magavana wengine nao wanasemekana kupendelea kuishi katika mikahawa ya kifahari wakati wanapokuwa Jijini Nairobi. Gavana kutoka eneo la magharibi anasemekana kuwa, majuzi alifikisha gharama ya matumizi katika hoteli moja mtaani Westlands, kuwa Sh5 milioni.

Magavana hawa wanasemekana kuwapokea wageni na kuandaa mikutano katika hoteli hizo, wakizipa biashara nzuri.

Afisa wa kaunti moja alieleza kuwa wanafika Jijini Nairobi angalau siku nne kila wiki, hali ambayo wanapendelea kutokana na marupurupu ya ziada ambayo wanapokea katika ziara hizo.

Lakini mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) alitetea wenzake akisema kuwa haiwezekani kwao kufanya kazi bila kufika Nairobi mara kwa mara.

“Ukweli ni kuwa hatujawahi kupata ugatuzi kamili. Bado tuko hatua za awali na hivyo huduma kadhaa za umuhimu bado ziko huko,” akasema Bw Oparanya.