Habari Mseto

Yafichuka walimu wanafundisha watoto kisiri

April 2nd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa baadhi ya walimu wanaendesha masomo ya ziada katika nyumbani zao, kwa malipo, na hivyo kuongeza uwezekano wa kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Hii ni kwa sababu kwa kuendesha mafunzo katika mazingira kama hayo vigumu kwa walimu hao kudumisha kanuni au hitaji la mtu kuwa umbali wa angalau mita moja na nusu kutoka kwa mwingine.

Kanuni hii imewekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Wizara ya Afya nchini kama njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu hatari.

Kufikia Jumanne wiki hii ulikuwa umesababisha vifo vya zaidi ya watu 37,000 ulimwenguni huku zaidi ya watu 700,000 wakiambukizwa. Na kufikia Jumatatu jioni serikali ya Kenya ilikuwa imethibitisha maambukizi ya watu 50 huku idadi hii ikikisiwa kupanda hadi 10,000 kufikia mwishoni mwa Aprili, mwaka huu.

Hii ndio maana sasa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kimewaonya wanachama wake dhidi ya kushawishiwa na wazazi waendeshe masomo ya ziada katika nyumba zao baada ya kupata habari kwamba baadhi ya walimu sasa wamegeuza nyumba zao kuwa “madarasa” ya kuendeshea masomo ya ziada.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Hesbon Otieno anasema walimu watakaokubali shinikizo za wazazi kama hao wanajiweka katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria, kwani ni njia ya kusambaza virusi vya corona.

“Tumepata habari kuwa baadhi ya walimu wanashawishiwa na wazazi wawafunze watoto wao katika nyumbani zao, kwa malipo. Kwa kufanya hivi, wanajiweka katika hatari ya kupata virusi vya corona.

Wajiepushe na hatari kama hii na wawakinge wanafunzi dhidi ya kuambukizwa na virusi hivi,” anasema Bw Otieno, akiongeza kuwa walimu watakaopatikana wakiendesha mafunzo kama hayo watachukuliwa hatua za kisheria.

Kiongozi huyo wa Knut anaeleza kuwa serikali ilikatiza shughuli za masomo majuma mawili yaliyopita ili kuzuia mtagusano wa walimu na wanafunzi ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

“Tume ya Huduma za Walimu (TSC) imefanya vizuri kwa kuwaruhusi walimu kusalia manyumbani. Knut pia inawajali na haitawaruhusu kugeuza nyumba zenu kuwa vyumba vya kuendeshea mafunzo ya ziada,” anasema Bw Otieno.

Anawashauri wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanafuatiliwa mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) kupitia mitandaoni redio na kwenye runinga yake, Edu TV, “ili watoto hao waendelee kumakinika kimasomo.”

Itakumbukwa kuwa serikali ilipiga marufuku masomo ya ziada mnamo 2012 baada ya kubainika kuwa baadhi ya walimu waligeuza shughuli hiyo kuwa njia ya kujipatia pesa zaidi wala sio kuwasaidia wanafunzi wanyonge kimasomo au kukamilisha silabasi.

Baadhi ya wazazi nao walitumia masomo ya ziada kama kisingizio cha kukwepa wajibu wao kama walezi, washauri na waelekezi wa watoto wao hali ambayo imepelekea baadhi ya wanafunzi kuwa watundu.Matokeo mienendo kama hii yamekuwa kukithiri kwa visa vya utovu wa nidhamu ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa katika shule za upili, haswa muhula wa pili.

Katika uchunguzi ulioendeshwa na aliyekuwa jopo kazi lililoongozwa na mkuu wa mkoa wa kati Bi Claire Omollo mnamo 2016, ukosefu wa malezi na ushauri wa wazazi ni mojawapo ya sababu kuu zilichongia visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili mwaka huo.

Jumla ya shule 110 za upili ziliteketezwa mwaka huo, wahusika wakuu wakiwa wanafunzi.