Habari Mseto

Yaibuka aliyeuawa aliiba mbuzi wa mwalimu wake

September 11th, 2018 2 min read

MOHAMED AHMED NA HAMISI NGOWA

SASA imeibuka kuwa kijana aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi jijini Mombasa alikuwa amedaiwa kuiba mbuzi wa mwalimu ambaye aliwahi kumfundisha kwenye Madrasa.

Familia ya Maitha Omar ilimlaumu mwalimu huyo, Mohammed Kassim Karega kwa kuwaelekeza maafisa wa usalama nyumbani kwao Omar akidai alimuibia mbuzi wake.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, afisa huyo alikuwa ameandamana na afisa huyo aliyempiga risasi Omar akila nyumbani kwao eneo la Mtongwe.

Zahara Salim, mmoja wa walioshuhudia kisa hicho alisema baada ya afisa huyo kumpiga risasi kijana huyo aliondoka akisema “siye yeye.”

Kulingana na ripoti ya polisi, walikua wanawasaka wezi waliomuibia Bw Karega mbuzi zake wiki chache zilizopita.

Aidha, kulingana na shahidi kwenye kesi hiyo ya wizi wa mbuzi Bw Ngolo Baya, kijana huyo si miongoni mwa wale aliyewatambua katika ushahidi wake.

“Mimi ndiye nilienda kwa Bw Karega na kumtajia majina ya waliohusika na wizi huo lakini jana nilishtuka kusikia kuwa Omar ameuawa na kuhusishwa na wizi huo,” akasema Bw Baya.

Tulipompigia simu Bw Karega alikanusha kuwepo katika eneo hilo la tukio na kueleza waandishi wetu wapuuze ripoti hiyo akidai kuwa “tayari wamezungumza na familia ya marehemu na kuelewana.”

Kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo, jamaa wa Omar ndiye alihusika katika wizi huo. Familia ilisema kijana wao alipigwa risasi kimakosa baada ya maafisa kumfananisha na mwizi.Wakati huo huo, Bi Shenaz Swaleh ambaye alikuwa ndani ya nyumba hiyo wakati wa tukio alisema kuwa kijana huyo alipigwa risasi akiwa kwenye ukumbi wa nyumba hiyo.

Taarifa ya mashahidi kuhusiana na kuuawa kwa kijana huyo zilitofautiana na zile za polisi waliodai kijana huyo alipigwa risasi nje akijihami na panga.

Akizungumza na wanahabari katika kituo cha polisi cha Central, kamanda wa polisi kaunti ya Mombasa Johnston Ipara alidai kijana huyo alijaribu kumpiga polisi kwa panga ndiposa akapigwa risasi.

“Maafisa wa usalama walikuwa wanamfuatilia kijana huyo na walipofika mahali alikuwa amejificha, alichomoka na panga akiwa na nia ya kumpiga afisa huyo na hapo ndipo alipigwa risasi,” akasema Bw Ipara. Hata hivyo, msemaji wa familia hiyo Ali Sasabu iliwalaumu polisi kwa madai ya “uwongo” dhidi ya mpendwa wao.

“Tunasikia uchungu sana tukiona polisi wanaeleza uwongo na kujaribu kuonyesha kuwa hawana makosa. Kama jamii hapa tumekuwa katika msitari wa mbele kusaidia polisi kupambana na wahalifu lakini wameua kijana asiye na hatia,” akasema.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko alimmtaka mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji pamoja na Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet kuagiza uchunguzi ili afisa aliyehusika na mauaji hayo aadhibiwe.