Habari MsetoSiasa

Yaibuka BBI sasa itachukua mkondo wa 'Punguza Mizigo'

December 5th, 2019 2 min read

Na JUTUS OCHIENG

MGONGANO unanukia kati ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wanasiasa wanaovumisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kuhusu mipango ya kukusanya sahihi milioni moja ili kusukuma ajenda ya mabadiliko ya katiba.

Kinaya ni kwamba mabadiliko hayo yanapendekeza kubuniwa kwa tume mpya ya uchaguzi, ilhali ni makamishina wa sasa wanaotarajiwa kuamua iwapo sahihi zitakazokusanywa zitafika idadi hitajika ya wapigakura milioni moja.

Ni suala hilo ambalo lilijadiliwa Jumanne wakati wa mkutano kati ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru katika afisi ya waziri huyo mkuu wa zamani ya Capitol Hill jijini Nairobi.

Bi Waiguru alisema safari ya BBI itaanza na raia kupokea mafunzo kuhusu ripoti hiyo, saini milioni moja zikusanywe, IEBC ithibitishe saini hizo ndipo zipelekwe kwa mabunge 24 ya kaunti ili kupitishwa na kupelekwa kwa Bunge la Kitaifa kupigiwa kura na wabunge.

“Tutahitaji uungwaji mkono wa nusu ya idadi ya wabunge pekee ili kuhakikisha BBI inatekelezwa bila kupitia kura ya maamuzi,” akasema Bi Waiguru.

Hata hivyo, haijabainika iwapo matamshi yake ni ya kulegeza msimamo kuhusu kuvumishwa kwa kura ya maamuzi ambayo imezua mgawanyiko kati ya wanasiasa nchini.

Kizungumkuti hasa ni vipi IEBC itakagua na kuidhinisha saini ambazo zitawafuta kazi Mwenyekiti Wafula Chebukati, makamishina Prof Abdi Guliye na Boya Molu.Hii ni baada ya waliokuwa makamishina Connie Maina, Margaret Mwachanya, Paul Kurgat na Roselyn Akombe kujiuzulu kutoka kwa tume hiyo.

Bw Chebukati wiki jana alikiri kwamba hajaisoma ripoti hiyo lakini akashikilia kwamba yeye pamoja na makamishina wengine wataendelea kuhudumu na hata kusimamia uchaguzi mkuu ujao hadi mikataba yao itamatike 2023.

“Ingawa sijapata muda wa kusoma ripoti ya BBI, kulingana nami tuliingia afisini 2017 na kipindi chetu cha kuhudumu kitakamilika Januari 2023. Sina shaka lolote kuhusu hilo,” akasema Bw Chebukati mjini Mombasa.

Bw Odinga alifichua kwamba mkutano wake na Bi Waiguru, ambaye amekuwa akirindima ngoma ya BBI, ulikuwa wenye nia ya kuhakikisha utangamano na umoja wa Wakenya.