Habari

Yaibuka corona pia inaathiri figo, moyo

July 15th, 2020 2 min read

WANDERI KAMAU na SAMMY WAWERU

IMEIBUKA kuwa virusi vya corona vinaathiri sehemu zingine za mwili, kinyume na dhana ambayo imekuwepo kuwa vinaathiri tu mapafu na viungo vingine vya kupumua.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema Jumanne kuwa matokeo mapya ya tafiti kadhaa zilizofanywa majuzi yameonyesha kuwa virusi hivyo vinaathiri pia figo, moyo na damu.

Kwenye kikao cha kila siku kuhusu hali ya virusi nchini jijini Nairobi, Dkt Mwangangi alisema kuwa hayo yalibainika baada ya watu kadhaa walioathiriwa vibaya kufanyiwa tafiti za kina.

“Kinyume na tulivyodhani siku 100 zilizopita kuwa virusi hivi vinaathiri kifua na mfumo wa kupumua katika binadamu, tafiti kadhaa katika sehemu mbalimbali duniani zimeonyesha kuwa vinaathiri figo, moyo na mzunguko wa damu mwilini kwa kuchelewesha mgando wake. Watu waliofanyiwa ukaguzi walipatikana na matatizo hayo licha ya kutokuwa nayo hapo awali,” akasema Dkt Mwangangi.

Alisisitiza kuwa ni jukumu la wale waliobainika kuambukizwa kutafuta matibabu kwa haraka.

“Ingawa tuna madaktari wenye ujuzi kuhusu matibabu ya virusi hivyo, ni muhimu wale wanaoonyesha dalili hizo kutafuta matibabu ya haraka ili kuepuka hali kama hizo,” akasema.

Kauli yake inajiri huku idadi ya watu walioambukizwa ikifika 10,791 baada ya watu 497 zaidi kuthibitishwa kuambukizwa jana.

Idadi ya wale waliofariki nayo ilifikia 202 baada ya watu watano kufariki, huku waliopona wakifikia 3,017 baada ya 71 kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Nayo idadi ya wahudumu wa afya walioambukizwa pia iliendelea kuongezeka, ambapo kufikia jana, wahudumu 450 kote nchini walikuwa wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Matibabu, Dkt Patrick Amoth, alisema kuwa 414 kati yao hawaonyeshi dalili hizo, hivyo wataendelea kupokea matibabu nyumbani.

Wahudumu wa afya nchini wamekuwa wakiishinikiza serikali kuweka mikakati ya kuwapa vifaa vifaavyo vya kujilinda, baada ya daktari mmoja na wauguzi wawili kufariki baada ya kuambukizwa.

Dkt Doreen Adisa, aliyefariki kutokana na virusi, alizikwa Jumatatu nyumbani kwao katika Kaunti ya Bungoma.

Wizara imeeleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya Covid-19 katika Kaunti ya Nairobi.

Imeonya endapo wakazi hawatachukua tahadhari, huenda vituo vya afya Nairobi vikalemewa na idadi ya juu ya wagonjwa.

Katika kikao na waandishi wa habari, Dkt Mwangangi alidokeza kwamba kaunti ya Nairobi kufikia sasa imeandikisha visa 5,705 vya virusi vya corona.

Nairobi ndiyo inaongoza katika maambukizi ya Covid-19.

“Wasiwasi tulionao ni ongezeko la visa vya maambukizi Nairobi,” Dkt Mwangangi akasema.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, Nairobi inafuatwa na Mombasa ambayo kufikia Jumanne ilikuwa imeandikisha visa 1,739.

Kaunti ya Busia ina visa 550 nayo Kiambu 520. Kufikia jana Jumanne, Kenya ilikuwa na jumla ya visa 10,791 baada ya visa vipya 497 kuthibitishwa.

Wizara ya Afya imeendelea kuhimiza Wakenya kuonyesha upendo kwa wagonjwa wa Covid-19 na pia waliopona, badala ya kuwatenga.

“Ugonjwa huu hausazi yeyote. Tunaendelea kupokea malalamishi kwamba kuna baadhi ya Wakenya wanaotenga wagonjwa na pia waliopona, tuondoe unyanyapaa,” Dkt Mwangangi akasema, akionya wanaopiga picha wagonjwa au waliopona na kuzipakia kwenye mitandao.

“Kuwafichua si mbinu ya kupambana na ugonjwa huu. Ni ugonjwa kama mengine. Unyanyapaa kwa waathiriwa hatutauruhusu,” Waziri akaeleza.