Habari MsetoSiasa

Yaibuka Kibaki alitumia pesa za mlipa ushuru kufadhili masomo ya jamaa zake

October 2nd, 2018 1 min read

Na David Mwere

IMEIBUKA kwamba Rais Mstaafu Mwai Kibaki alitumia nafasi yake kama rais kushinikiza kufadhiliwa kwa masomo ya jamaa zake wa karibu wakati akihudumu kama rais.

Kwenye mahojiano na Kamati ya Uhasibu ya Bunge Jumanne, aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura, alisema kuwa Bw Kibaki alimwagiza kuhakikisha kwamba watoto wawili wa mpwaye, Philip Githinji wamepata ufadhili wa serikali kusomea nchini Australia.

Hilo lilipelekea serikali kulipa Sh25 milioni kwa ufadhili wa Ian Githinji na Sandra Githinji kupokea masomo yao katika Taasisi ya Teknolojia ya Melbourne nchini Australia.

Kamati hiyo ilishangaa ni kwa nini wawili hao hawangesomea nchini. Na japo walikuwa wamepangiwa kusoma kwa miaka minne pekee, walijisajili kusoma kwa miaka sita. Hadi sasa, wangali hawajamaliza masomo yao.

Kulingana na Bw Muthaura, Bw Kibaki alimwangiza kushirikiana na aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Elimu Prof Chrispus Kiamba kuhakikisha wanafunzi hao wamepata usaidizi baada ya baba yao kupoteza kazi.

“Hangeweza kugharamia masomo ya babake baada ya kupoteza kazi yake,” akasema.

Bw Muthaura alisema kuwa Bw Githinji aliomba msaada serikali kumsaidia kupitia mpango wa kuwafadhili wanafunzi. Alisema kuwa Bw Kibaki alikubali ombi lake, ambapo aliiagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha ombi hilo limetekelezwa kikamilifu.