Yaibuka raia wa Amerika aliteswa kisha kuuawa

Yaibuka raia wa Amerika aliteswa kisha kuuawa

Na MARY WAMBUI

RIPOTI ya upasuaji wa mwili wa mfanyabiashara mwenye asili ya Kisomali na Amerika, Bashir Mohamoud, imefichua kwamba kifo chake kilitokana na kunyongwa.

Wakili wa marehemu Bashir, Charles Madowo, alisema mwendazake aliteswa kabla ya kuuawa na kisha kutupwa kwenye Mto Nyamindi, eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga.

Alisema mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha yaliyotokana na kifaa butu na kuchomwa katika sehemu mbalimbali.

“Kiini hasa cha kifo kulingana na ripoti ni kunyongwa, lakini pia kuna ushahidi kwenye mwili wake kwamba aliteswa.

“Kuna majeraha kichwani yanayoonyesha aligongwa kwa kifaa butu, majeraha ya kuchomwa na kuumizwa kwenye vidole na kucha zake,” alisema Bw Madowo.

Shughuli hiyo ya upasuaji ilichukua muda wa zaidi ya saa moja ikiongozwa na Mpasuaji Mkuu wa Serikali, Johansen Oduor na kushuhudiwa na wapasuaji wengine wawili wa kibinafsi, Bw Madowo, makachero wa DCI na mwakilishi wa familia.

Chembechembe zilichukuliwa pia kutoka kwa mwili wa marehemu ili kufanyiwa uchunguzi zaidi katika maabara ya serikali.

“Tunachotumai ni kuwa uchunguzi wa kina utafanyika na watu waliohusika watakamatwa na kushtakiwa,” alisema wakili huyo.

Mwili wa Bashir ulizikwa jana katika makaburi ya Kiislamu ya Lang’ata baada ya maombi katika Msikiti wa Masjid Salaam, South ‘C’.

“Hatutawahi kuwasamehe wale waliomuua Bashir na tunamwomba Mungu awaadhibu watu wanaomwaga damu isiyo na hatia,” alisema Rashid Ali Omar, ambaye ni baba-mkwe wa mwendazake.

You can share this post!

Pambano kali kushuhudiwa Kiambu Ruto akikabili Uhuru

Kampuni za mikate zaonywa dhidi ya kupotosha wateja kuhusu...