Yaibuka Ruto aligawia Jumwa GSU wawili ilhali ana kesi

Yaibuka Ruto aligawia Jumwa GSU wawili ilhali ana kesi

Na IBRAHIM ORUKO

NAIBU Rais William Ruto, amesemekana alimpa Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, maafisa wawili wa polisi wenye taaluma ya hali ya juu ya kulinda watu mashuhuri wakati serikali ilipompokonya mbunge huyo walinzi wake miaka michache iliyopita.

Duru ziliambia Taifa Leo kuwa, hatua hiyo ambayo pia Dkt Ruto amesemekana alimfanyia Mbunge wa Kapsaret, Bw Oscar Sudi, ni mojawapo ya sababu zilizopelekea serikali kumpokonya baadhi ya walinzi wake wa kikosi cha GSU.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i aliambia kamati ya bunge kwamba, Naibu Rais alijitwika jukumu la kuwahamisha maafisa ambao serikali ilimpa kwa ulinzi wake.

Duru zilizohudhuria kikao cha faraghani kati ya Dkt Matiang’i na Kamati ya Bunge ya Usalama na Usimamizi wa Kitaifa, ziliambia Taifa Leo kuwa, waziri alimkashifu Dkt Ruto kwa kutuma polisi wakalinde watu ambao aliwataja kuwa “wahalifu na wengine ambao mienendo yao ni ya kutiliwa shaka, ambao ni hatari kwa usalama wa taifa”.

“Inspekta Jenerali wa Polisi pekee ndiye ana mamlaka ya kuhamisha maafisa wa polisi, na haiwezekani kukubaliwa kuwa watu wengine wawe wanajitwika mamlaka hayo,” Dkt Matiang’i alisemekana kuwaambia wabunge.

Baadhi ya maafisa wa GSU waliondolewa katika kikosi kinacholinda nyumba za naibu rais, na mahala pao pakachukuliwa na kikosi cha Polisi wa Utawala ambao hulinda rasilimali muhimu na majengo ya serikali.

Bi Jumwa na Bw Sudi, ambao ni miongoni mwa wabunge wanaoegemea upande wa Dkt Ruto, walipokonywa ulinzi unaopeanwa kwa wabunge wakati waliposhtakiwa kwa uhalifu.

Bi Jumwa alishtakiwa kwa madai ya mauaji, naye Bw Sudi akashtakiwa kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi.

Katika kesi ya Bi Jumwa, amedaiwa alihusika katika mauaji ya Ngumbao Jola, wakati vurugu zilipotokea kabla ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Wadi ya Ganda, Kaunti ya Kilifi mnamo Oktoba 15, 2019.

Alikanusha mashtaka, na kesi hiyo ingali inaendelea mahakamani Mombasa.Kando na kesi inayohusu uchochezi, Bw Sudi alishtakiwa pia kwa madai ya kughushi vyeti vyake vya elimu.

“Maafisa hao huwa wamepokea mafunzo ya hali ya juu ili kulinda watu mashuhuri na wenye hadhi ya juu zaidi, lakini mtu alitumia nafasi yake vibaya, akawatumia vibaya kwa vile anajua wana nidhamu sana na hawawezi kulalamika wanapoamrishwa,” imesemekana Dkt Matiang’i aliambia wabunge.

Hata hivyo, Naibu Rais kupitia kwa katibu wake wa mawasiliano, Bw David Mugonyi, alikanusha madai hayo.“Naibu Rais huwa hajipatii maafisa wa usalama wala kupeana kwa mtu mwingine yeyote,” akasema Bw Mugonyi, kupitia kwa taarifa kwa vyumba vya habari.

Jana, Dkt Ruto alimkashifu Dkt Matiang’i akidai ameingiza mzaha katika suala hilo la usalama huku akiuliza kwa nini hatua hizo za kumbadilishia walinzi zilisubiri hadi sasa.

Akihutubia wanasiasa kutoka Kaunti ya Nakuru wanaotarajia kuwania tikiti za Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa uchaguzi ujao nyumbani kwake Karen, Nairobi, Ruto alisisitiza kuwa yaliyojiri ni sehemu ya vita anavyopigwa na mahasimu wake wanaotaka asimrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

You can share this post!

Ninauza mayai ya Sh1.5m kila siku – Ruto

Polisi 6 wakanusha mauaji ya ndugu wawili wa Kianjokoma