HabariSiasa

Yaibuka Ruto anadunishwa na wadogo wake

April 25th, 2019 1 min read

Na VITALIS KIMUTAI

WABUNGE wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto katika ukanda wa Bonde la Ufa wamelalama kwamba anadunishwa na baadhi ya maafisa serikalini.

Wabunge walidai kuwa maafisa hao wamekuwa wakikwepa kuhudhuria hafla zake kimakusudi, jambo walilotaja kama kumkosea heshima.

Wabunge hao, waliojumuisha Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho), Christopher Lagat (Bomet), wabunge Japheth Mutai (Bureti) na Hillary Koskei (Kipkelion Magharibi) walisema maafisa hao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao.

Wakizungumza katika eneo la Bureti, Kaunti ya Kericho, viongozi hao walitishia kuwang’oa mamlakani maafisa hao, kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao.

“Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya mawaziri, makatibu na wakuu wa mashirika ya serikali ambao wamekuwa wakifanya mikutano ya usiku kupanga vile watamwangusha Dkt Ruto, ili kuhakikisha kuwa hatamrithi Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa 2022,” akasema Bw Cheruiyot.

Akaongeza: “Ninataka kuwaambia kwamba tutawasilisha hoja ya kutokuwa na imani nao. Hatuwezi kukaa kitako huku Naibu Rais akiendelea kukosewa heshima.”

Kwa upande wake, Bw Koskei alimkashifu vikali Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli kwa kauli yake kuwa, jina la Dkt Ruto halitakuwa debeni kwenye uchaguzi huo.

“Unaweza kuwa humpendi Dkt Ruto, lakini lazima uelewe kuwa ndiye Naibu Rais, ambapo afisi yake lazima iheshimiwe,” akasema mbunge huyo, katika kauli iliyoonekana pia kuwalenga maafisa hao.

Bw Mutai alisema malumbano ya kisiasa katika Chama cha Jubilee (JP) yanapaswa kukomeshwa, kwa kuwa yanaathiri sana utekelezaji wa miradi muhimu ya serikali.

Hata hivyo, mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter amepuuzilia mbali kauli za wenzake kwamba kuna mgawanyiko katika JP.

“Tuliwaambia viongozi wetu kwamba yalikuwa makosa makubwa kuvunja chama cha URP na kukiunganisha na TNA. Kwa sasa, waliotulaumu kwa msimamo wetu wanalalama,” akasema.