Habari Mseto

Yaibuka serikali inapanga kutumia Sh10b kununua treni zilizotumika

February 24th, 2019 2 min read

Na Edwin Okoth

KENYA inapanga kutumia Sh10 bilioni kununua magari moshi 11 kuukuu, yaliyotumika hadi kwa miaka 25 kutoka Uhispania pamoja na mabasi ya hadhi, katika mpango wa kurahisisha usafiri Jijini Nairobi.

Magari hayo, ambayo aidha yanaripotiwa kuwa ya kiwango cha chini na yenye injini hafifu yanatarajiwa kuwasili nchini kuanzia Juni mwaka huu, wakati hata njia za usafiri wa reli hazijaundwa.

Habari kuhusu ununuzi huo ziko katika ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na washauri wa kimataifa waliopewa kazi na Shirika la Reli, japo nyingi zimefichwa zisifichuke kwa umma.

Taifa Jumapili imebaini kuwa sasa, mpango wa kuleta magari hayo umepiga hatua kadha na kuwa unasukumwa na maafisa fulani wenye usemi katika wizara ya Uchukuzi, licha ya changamoto za utendakazi kutajwa.

Timu inayoshughulikia suala hilo ilianza kwa kuishauri wizara hiyo kuingia katika biashara hiyo na serikali ya Uhispania, hatua ambayo ilizuia mpango huo wa ununuzi kukaguliwa.

Maafisa wakuu katika wizara hiyo, wakiwemo waziri James Macharia na makatibu katika wizara hiyo, Bw Charles Hinga na Bi Esther Koimett, wamekuwa wakikwepa kuzungumzia suala hilo la ununuzi wa magari moshi yaliyotumika kwa hadi miaka 25, licha ya hatari iliyopo kuwa huenda pesa za mlipa ushuru zikatumbukia shimoni.

Kenya inauziwa magari moshi hayo kwa kati ya Sh71 milioni na Sh137 milioni, jinsi yalivyo.

Ripoti hiyo ilikuwa imependekeza mpango ambao ungeifaa Kenya kwa muda mrefu, kwa kununua magari moshi na mabasi ambayo hata yangewavutia watu wanaomiliki magari kutumia mbinu hizo za usafiri.

Ripoti hiyo ilipendekeza idadi ya watu wa kubebwa na treni, namna ya reli kujengwa na mahali zingepitia ili kuhudumia wakazi wengi wa Jiji.

Hata hivyo, ziara iliyofanywa na maafisa wa shirika la reli na wizara wakiongozwa na Bi Koimett na Bw Hinga kuelekea Uhispania ilibadili mkondo wa mambo, kwani walipuuzilia mapendekezo ya ripoti na kuamua kuendelea na mpango huo wa kununua treni hizo.

“Baada ya ziara hiyo ya Uhispania, mapendekezo hayo hayakuwa na umuhimu tena. Baadhi ya maafisa wa wizara walijitenga na maafisa waliokuwa wameenda pamoja Uhispania na hata kuanza kupiga simu Kenya, siku mbili tu baada ya maafisa wa usafiri wa reli Uhispania kuzungumza, Jijini Barcelona,” afisa aliyekuwa katika ziara hiyo ya Septemba 6-15 akaeleza Taifa jumapili.

Ziara hiyo haikulenga kuwa ya ununuzi wa treni, lakini wiki mbili baadaye, wizara ilifanya uamuzi wa kuzinunua.

Wizara hiyo, mnamo Desemba 5 iliitaka wizara ya Fedha kuitengea Sh10 bilioni za kujenga reli na kuboresha zilizopo sasa, mbali na kununua treni hizo na mabasi ya kisasa.

Licha ya changamoto hizi, Bw Hinga alisema kuwa habari zitatolewa tu baada ya mchakato wa ununuzi kukamilika.

“Tuko katika zoezi la kupeana kandarasi na kununua kwa hivyo habari zitatolewa baada ya zoezi hili kukamilika,” akasema.